2015-03-18

Ina sikitisha sana:Mamia ya wakazi wa Mwanza wamzika Marsh

 
Wachezaji wa Marsh Athletics wakiangua kilio wakati wa kuagan mwili wa marehemu Sylvester Marsh, kwenye eneo la Mirongo jijini Mwanza jana. Marsh alikuwa mmiliki wa kituo hicho cha kukuza vipaji.
 
Shughuli za kuaga mwili wa kocha huyo zilianza saa 4 asubuhi kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mirongo kadri muda ulivyokuwa unakwenda ndipo waombolezaji walizidi kumiminika katika eneo hilo.

Mwanza. Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo aliwaongoza mamia ya wakazi wa jiji hili katika mazishi ya kocha wa zamani wa Taifa Stars na mkurugenzi wa kituo cha Marsh Athletics, Sylvester Marsh aliyezikwa jana katika makaburi ya Igoma.

Shughuli za kuaga mwili wa kocha huyo zilianza saa 4 asubuhi kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mirongo kadri muda ulivyokuwa unakwenda ndipo waombolezaji walizidi kumiminika katika eneo hilo. 

Viongozi na waombolezaji waliofika uwanjani hapo walishindwa kujizuia kutoa machozi baada ya nahodha wa Marsh Athletics, Bernad Pastory kusoma risala juu ya mchango wa marehemu katika kuendesha timu hiyo.

Mkuu wa mkoa Mulongo alisema katika kumuenzi kocha huyo kila mwaka kutakuwa na mashindano yanayojulikana kwa jina la Marsh pamoja na kuhakikisha kituo hicho cha michezo alichokiacha kocha huyo kinaendelezwa.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Salum Madadi alisema kifo cha kocha huyo ni pigo kubwa kwa shirikisho hilo kwani alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakimtegemea katika kuinua na kuboresha soka la Tanzania haswa kwa vijana chini ya miaka 17. 


“Tutaenzi hii academy aliyoacha marehemu na hili liko chini ya idara yangu tutahakikisha tunaiendeleza kwa sababu tunatambua mchango wa kocha huyu katika soka la Tanzania,”alisema Madadi.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani Mwanza(MZFA), Jackson Songola alisema Mwanza imepoteza mtu muhimu aliyepigania kuinua soka la mkoa huo.

Mtoto wa kwanza wa marehemu Wayne Marsh alisema kifo cha baba yake kimemwacha njia panda kwani hajajua nani ataweza kumsomesha kwani walikuwa wakimtegemea marehemu kwa kila kitu.
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...