MTU mmoja aliyefahamika kwa majina ya Donald Peter Mwakajonga (62) mkazi wa Kijiji cha Mkunga wilayani Rungwe, Mbeya ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani kwa kile kinachodaiwa kuwa ni imani za kishirikina.
Habari kutoka kijijini hapo zinasema mwili wa Mwakajonga ulikutwa na majirani ukiwa nje ya nyumba yake.
“Mwili wake ulikutwa ukiwa nje ya nyumba yake hapa Kata ya Mkunga, Tarafa ya Ukukwe, wilayani Rungwe Jumapili iliyopita, saa moja na dakika hamsini asubuhi. Kwa kweli sisi tulishangazwa lakini inasemekana aliuawa kutokana na imani za kishirikina,” alisema shuhuda mmoja mwenyeji wa kijiji hicho aliyeomba jina lake kuhifadhiwa kwa kile alichodai ni kutokana na usalama wake.
Aliongeza kudai kuwa, kuna baadhi ya watu walikuwa wakimsema mzee Mwakajonga kwamba ni mchawi alikuwa akiwaroga wanakijiji na anaamini kwamba watu hao ndiyo waliomuua.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, SACP Ahmed Msangi alipozungumza na gazeti hili, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.
“Ni kweli tukio hilo limetokea na inadaiwa kuwa chanzo cha kifo cha mtu huyo ni kipigo kilichotokana na imani za kishirikina,” alisema Kamanda Msangi.Alipoulizwa kama kuna mshukiwa yeyote ambaye amekamatwa hadi sasa alijibu:
“Mpaka sasa tunamshikilia mtuhumiwa mmoja aitwaye Daniel Venance mwenye umri wa miaka 35, mkazi wa kijiji hicho alichofia marehemu na kutokana na tukio hilo sisi jeshi la polisi tunaendelea na uchunguzi wetu.”
Kamanda Msangi aliwataka wananchi kuachana na tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake akasema kama kuna mtu wanamhisi kutenda maovu waliarifu jeshi la polisi ili aweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria baada ya kufanyika uchunguzi.
Kamanda Msangi aliwataka wananchi kuachana na tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake akasema kama kuna mtu wanamhisi kutenda maovu waliarifu jeshi la polisi ili aweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria baada ya kufanyika uchunguzi.
0 comments:
Post a Comment