2015-03-19

Bidhaa za China zinavyotamba kwenye soko la Tanzania



Wiki mbili zilizopita katika sehemu ya kwanza ya makala haya ya ‘Dar hadi China’ tuliona jinsi wakuu wa mataifa haya mahili wanavyoimarisha uhusiano na kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara wa mataifa haya mawili. Tukaona pia umuhimu wa wafanyabiashara pande zote kuwa huru katika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.


Leo tunakutana na wafanyabiashara wa Tanzania wanaelezea juu ya kile ambacho kinawavutia katika kununua na kuuza bidhaa za China. Yamekuwapo maneno mengi kuhusu bidhaa za China.


Wafanyabiashara na wanunuzi wa Tanzania wana nini cha kusema?


Ushindani wa bidhaa mbalimbali za biashara, zikiwapo zinazotoka nje ya nchi, unazidi kukua siku hadi siku nchini.


Kila kukicha wafanyabiashara wanaumiza vichwa jinsi ya kumudu ushindani huo kwa kubuni mbinu mbalimbali za kuwavutia wateja wao.


Kutokana na ushindani huo, wafanyabiashara hutafuta bidhaa zinazopendwa na wateja wengi. bidhaa hizo, huzinunua kutoka kwa wazalishaji wa ndani na nje.


Miongoni mwa mataifa ya nje ambayo bidhaa zake huingizwa na kuuzwa kwa wingi nchini ni China.


Kariakoo ni eneo kuu la biashara nchini ambalo linategemewa na mikoa yote nchini kupata bidhaa mbalimbali. Ni eneo ambalo twaweza kusema ni lango la kuingiza bidhaa za aina mbalimbali nchini kwa kuwa wafanyabiashara wa mikoani hununua vitu na kwenda kuviuza wanakotoka.


Eneo la Kariakoo lililopo Jijini Dar es Salaam, linaelezwa kuwa na asilimia kubwa ya bidhaa zinatoka China. Hizi ni kama vile nguo, viatu, mapambo, vifaa vya umeme, ujenzi, michezo, pikipiki, bajaji na samani. Bidhaa hizi zinatumiwa na Watanzania wengi.


Bob Lema ni mfanyabiashara katika soko hilo. Amekuwa akifanya biashara ya kuuza vifaa vya umeme kwa kipindi cha miaka 10 sasa. Anasema uzoefu wake katika biashara hiyo unaonyesha kuwa bidhaa nyingi zinazoingizwa kutoka nje ni zile za China.


“Tunanunua bidhaa kutoka nchi mbalimbali, lakini China inaongoza. Huo ni mtazamo wangu na jinsi ninavyofahamu soko la biashara lilivyo hasa hapa Kariakoo,” anasema Lema huku alionyesha baadhi ya vifaa vya umeme alivyonunua kutoka China.


“Unaona kama hizi spika, zinaitwa ‘skeleton speakers’ zipo za Marekani na China. Lakini palee (anaonyoshea nyingine) zile ni za China. Halafu kuna televisheni zote hizo zinatoka China.”

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...