Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akiwasalimia wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya mjini Dodoma na waendesha bodaboda walioandamana kwenda nyumbani kwake mjini humo jana kwa ajili ya kumshawishi achukue fomu ya kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Picha na Anthony Siame
Arusha/Dodoma/Mbeya. Kadri uchaguzi mkuu unavyokaribia ndivyo makundi mbalimbali ya jamii yanavyoibuka kwa staili tofauti za kuwashawishi baadhi ya makada ili watangaze nia ya kuwania urais ndani ya CCM.
Makundi hayo yalianza kwa kumshawishi Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na sasa yameibuka mengine katika mikoa ya Mbeya na Arusha yakiwashawishi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Hata hivyo makundi hayo yameelezwa na mmoja wa watu waliotangaza kuwania nafasi hiyo kuwa ni mbinu ya kimaigizo ya baadhi ya wagombea kujitangaza kwa kuyaandaa na kuyalipa posho.
Wanafunzi watinga kwa Lowassa
Siku moja baada ya kuwapokea masheikh 50 kutoka Bagamoyo, jana mbunge huyo alipokea makundi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, madereva wa pikipiki (bodaboda) na wamachinga wa Dodoma wakimtaka achukue fomu kuwania nafasi hiyo.
Tayari mbunge hiyo alishampokea Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Dk Rapahel Chegeni na baadaye kundi marafiki wa Lowassa kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Wanafunzi hao ambao waliongozana na baadhi ya wahadhiri walitoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), St John, Mipango na Chuo cha Biashara (CBE), Tawi la Dodoma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti nyumbani kwake mjini hapa jana, wanafunzi hao walimtaka Lowassa kuchukua fomu ya kuwania urais wakati utakapofika.
“Sisi hatutafuni maneno, ni watu wawazi na tuna tamaa kwa mtu ambaye tuna matumaini naye na mtu ambaye tuna matumaini naye ni wewe Lowassa,” alisema Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wazazi la CCM Kusini Unguja, Haji Amiri na kuongeza:
“Watanzania wana matumaini na wewe. Sasa yeyote anayetaka kuyafunika matumaini yale ni sawa na kukiuka matumaini yetu.”
Kiongozi wa madereva Bodaboda, Bakari Ndalama alisema yeye na wenzake walifika kumuomba kugombea nafasi hiyo kwa sababu akichukua, hali ya ajira itakuwa nzuri.
“Wewe umekuwa ukilisemea jambo hili mara kwa mara. Ukipata urais ajira zitakuwa nzuri kwa vijana,” alisema Ndalama.
0 comments:
Post a Comment