2015-03-23

Zitto apata mrithi PAC



  Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Amina Mwidau ameteuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).

Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Amina Mwidau amerithi mikoba ya aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe baada ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa kamati ya Hesabu za Serikai(PAC).

Kabla ya kujiuzulu ubunge Ijumaa iliyopita, Zitto alikuwa mwenyekiti wa kamati hiyo.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana, uchaguzi huo ulifanyika jana mchana katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Chanzo cha habari, kimesema nafasi hiyo iligombewa na mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Lucy Owenya ambaye aliambulia kura mbili kati ya 17 zilizopigwa katika uchaguzi huo.

Amina aliibuka mshindi baada ya kuzoa kura 15 katika uchaguzi huo.

Wajumbe ambao hawakuwapo kwenye uchaguzi huo ni wabunge wa Viti maalumu, Easter Matiku (Chadema) na Catherine Magige (CCM) na Mbunge wa Magogoni, Kombo Khamis Kombo.

Alipoulizwa kuhusu uchaguzi huo, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema hana taarifa za kufanyika kwa uchaguzi huo.

“Hata sijui kama kuna uchaguzi umefanyika leo wa kamati yoyote,” alisema Joel ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge.

Akizungumza na gazeti hili jana jioni, Amina alisema ataendeleza pale alipoishia Zitto na Watanzania wategemee uwazi zaidi katika utekelezaji wa kazi za kamati hiyo.
“Kamati hii ina action plan (mpango kazi) ambao imepanga kuufanyia kazi, kwa hiyo nitaangalia pale alipoishia Zitto na mimi nitaendeleza,”alisema Amina.

Alipoulizwa kuhusu changamoto, alisema kazi itakuwa rahisi kutokana na ushirikiano na umoja walionao wajumbe wa kamati hiyo.

“Sisi katika kamati tulikuwa wapinzani watano tu wengine wote ni kutoka CCM, lakini kwa ushirikiano na umoja tulioujenga ndani ya kamati, wakati mwingine huwa tunasahau kabisa kama tunatoka kama vyama tofauti, naahidi kuendeleza na kuusimamia umoja huo,” alisema Amina.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...