
Watu wanne akiwemo Mweyekiti wa Kijiji cha Ihanda tarafa ya Mlali wilayani Kongwa mkoani Dodoma wanashikiliwa na Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kushiriki katika mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Kamishna msaidizi Mwandamizi wa Polisi David Misime, vikongwe watatu waliuawa Machi Mosi mwaka huu kwa madai ya kushiriki kuzuia mvua isinyeshe kijijini hapo kwa njia za kishirikina.
Vikongwe hao ni pamoja na Saidia Chakutwanga mwenye umri wa miaka 80 wa kijiji cha Masinyeti aliyeuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali pamoja na mtu na mkewe Peter Kaluli mwenye umri wa miaka 85 na Laila Kaluli mwenye umri wa miaka 80 wote wa kijiji cha Masinyeti Tarafa ya Mlali wilayani Kongwa nje ya mkoa wa Dodoma.
Kamanda Misime amesema bado taarifa zaidi zinahitajika katika jitihada dhidi ya mapambano hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama anazitaka kamati za ulinzi na usalama za vijiji kufanya jitihada za kuwabaini wahusika wote.
Vitendo vya mauaji ya wazee vimezidi kuongezeka na kusambaa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Takwimu kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Serikali zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 1998 – 2001 kulikuwepo na matukio 17,220 ya kuwadhalilisha wazee na mauaji 1,746 kutokana na imani za kishirikina.
Ripoti ya kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC ya mwaka 2009 ilionyesha kuwa wanawake wazee 2,583 walikuwa wameuawa katika mikoa minane ikiwa ni wastani wa mauaji 517 kila mwaka.
0 comments:
Post a Comment