Shoga, ni matumaini yangu hali yako ipo poa na unaendelea kusaka ugali wa kula watoto kama kawaida.
Kwa upande wangu namshukuru Mwenyezi Mungu, afya yangu, wanangu na mume wangu ni nzuri kabisa.
Baada ya wiki iliyopita kuzungumza nawe kuhusu kuyafanyia kazi yote uliyofundishwa na kungwi wako ili umpagawishe mumeo na kumfanya atulie nyumbani, leo nimekuandalia kitu tofauti.
Nafanya hivyo ili kuufungua ubongo wako katika suala zima la mapenzi, lengo likiwa tusiwakwaze wenza wetu kwa namna yoyote pia kuzilinda ndoa zetu zisijevamiwa na viruka njia vinavyopenda kuruka na waume za watu.
Shoga, kama kichwa kilichopo hapo juu kinavyojinadi, usikubaliane kabisa na suala la mumeo ‘kukenua’ meno na rafiki zako mpaka kufikia hatua ya kuonesha jino lake la mwisho.
Nasema hivyo kwa sababu tabia ya kumuacha mumeo akipiga stori na shoga yako huku wakigongesha viganja kwa madai ni mtu na shemeji yake, itakuja kukuletea balaa katika ndoa yako.
Wapo wenzetu ambao wamejikuta wakiporwa waume zao kisa kikiwa ni tabia ya kuwaacha waume zao wawe karibu na marafiki zao ambao walitumia mpenyo huo kuwanyakua.Shoga yangu, hakuna jambo la hatari katika uhusiano wa wa wawili wapendanao kama mwanamke kumpa uhuru mwenza wake wa kupiga stori kwa muda mrefu na shoga zake, kutoka ‘out’ kwa mwamvuli wa shemeji yake.
Kufanya hivyo ni sawa na kumuachia simba mbuzi ambaye iwe na isiwe atamla tena bila kufanya kazi ngumu kwani atakuwa kaingia katika anga zake mwenyewe.Shoga, baada ya rafiki yako kuanza kukuibia mali zako kitakachofuatia ni mambo mawili, kukudharau au kuzidisha upendo wa bandia kwako ili aendelee kula vitamu visivyoisha hamu vya mumeo.
Kama walivyosema wahenga kwamba mtu akinogewa na utamu wa asali ataamua kuchonga mzinga ambapo bila huruma atakupora mumeo bila kujali kama unaishi naye kinyumba au ulifunganaye ndoa.
Kuepuka madhara ya kuporwa mume uliyetokanaye mbali, ukimuona mumeo anawazoea sana marafiki zako mpige ‘stop’ ili kuunusuru uhusiano wenu kama siyo ndoa. Ni aibu kwa mwanamke kuporwa mume na rafiki yake kwa kuzembea kumuacha wa ubani wake akicheka na kushikana mwilini na shoga zake.Bye!
GPL
0 comments:
Post a Comment