2015-03-23

Vijana wafurika kwa Lowassa kumtaka agombee urais


Wanafunzi
Na Fredy Azzah, Dodoma
VIJANA zaidi ya 300 ambao ni wawakilishi wa wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Dodoma, waendesha bodaboda na wamachinga, wamefika nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kumtaka agombee urais.

Vijana hao walifika nyumbani kwa Lowassa eneo la Area C saa 5.00 wakitembea kwa miguu wakiongozwa na bodaboda.

Baadhi yao walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na ujumbe tofauti ukiwamo“4U Movement, wanavyuo, Chuo Kikuu Dodoma, Shule za Kata ni vielezo vya uchapakazi wako, wewe ndiye rais wetu wa suluhu ya ajira mwaka 2015.”

Bango jingine liliandikwa: ‘Wanabodaboda Sheli Kisasa, Mheshimiwa Lowassa sisi tunakuunga mkono kama utaamua kugombea urais, chukua fomu tutalipia tuko na wewe’.
Jingine liliandikwa:‘4U Movement Friends of Lowassa, walitunyima elimu… ukatupatia shule za kata, CCM tupeni Lowassa nafasi ya urais 2015. utumishi, uwajibikaji, umoja na uzalendo’

Baada ya kupokewa na Lowassa, wawakilishi wa makundi hayo walieleza lengo la ziara yao ambako mwakilishi wa wafanyabiashara ndogondogo (machinga), Robert Mwakasele, alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na kauli mbalimbali za mbunge huyo wa Monduli zinazoonyesha kuwa anajali matatizo ya vijana.

“Kauli kama ‘ajira kwa vijana ni bomu’ linalosuburi kulipuka ndizo zilizotusukuma, tuko wamachinga 400 tunakuomba ugombee muda utakapofika,”alisema.

Naye Bakari Ngalama ambaye aliwakilisha waendesha bodaboda alisema;“Tumekuja kukutaka ugombee kwa sababu tunajua ukiwa rais suala la ajira litapatiwa majibu.”

Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Fredrick Luterano, alisema Lowassa ni kati ya viongozi bora hivyo ni vema akachukua nafasi hiyo kuliongoza taifa.

Wakati vijana hao wakieleza hayo, Lowassa alisema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mgumu hivyo akawataka vijana hao kuhakikisha wanajiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura waweze kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu.

“Election is about numbers (uchaguzi ni namba), wakijiandikisha watu milioni 23 italeta tofauti kubwa sana.

Mnaonishawishi kugombea na mimi niwashawishi mkawashawishi watu wajiandikishe kupiga kura. 
Mtu asikudanganye wewe ukishapitwa namba pale ukajitia sijui amevuruga uchaguzi, sijui amehonga, hakuna chochote, na nyie muonyeshe mfano kwa kujiandikisha,”alisema.

Kabla ya vijana hao, wazee 21 kutoka Baraza la Wazazi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) walifika kwa Lowassa kumtaka agombee nafasi hiyo.

Wazee hao wakiongozwa Mwenyekiti wao, Dk. Damas Mukassa, walisema wanaamini Lowassa akishika nafasi hiyo atafanya vema.
Akijibu ombi lao, Lowassa alisema amekwisha kupokea maombi mbalimbali kama hayo, muda utakapofika kwa taratibu za chama ataona ni nini cha kufanya.

Huo ni mwendelezo wa watu wanaokwenda kumshawishi Lowassa agombee urais.
Mwishoni mwa wiki Masheikh 50 kutoka misikiti mbalimbali wilayani Bagamoyo mkoani Pwani walifika nyumbani kwake Dodoma kumshawishi agombee nafasi hiyo kubwa nchini.

Akijibu hoja za masheikh hao. Lowassa alisema muda wa kuchukua fomu ukifika atatekeleza matakwa hayo.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...