Akihubiri siku ya Pasaka katika Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship lililopo Mwenge katika Jiji la Dar-Es-Salaam, Askofu Mkuu Zachary Kakobe alisema kwamba, inajulikana wazi kwamba Lowassa amekuwa anautaka Urais kwa udi na uvumba kwa miaka mingi, hata mwaka 1995 alijitosa hadharani kuuwania, sasa anapodai kwamba hivi sasa kuna makundi yanayokwenda kwake kumshawishi agombee Urais, kana kwamba yeye hataki Urais, anakuwa anamdanganya nani?
Ingawa katika mahubiri hayo ya saa mbili, Kakobe hakumtaja Lowassa kwa jina, hata hivyo Kakobe alisema, "Wako watu wengine ambao inajulikana wazi kwamba wamekuwa wakiutaka Urais kwa udi na uvumba, kwa miaka mingi, lakini hivi sasa wanasema kuna makundi ya watu yanawafuata nyumbani, kuwashawishi kugombea Urais; kama vile hawautaki Urais, hivi watu hawa wanamdanganya nani?
"Na wale wanaokwenda kumshawishi mtu ambaye kwa miaka mingi, anajulikana kwamba anautaka Urais, hawajui kwamba nao wanafanywa kuwa wajinga? Mtu anayejulikana kwa muda mrefu kwamba anautaka Urais, ni vema akatangaza tu moja kwa moja nia yake, bila haja ya ghiliba."
Katika mahubiri yake yenye kichwa, "UPOTOSHAJI WA UKWELI", Kakobe alieleza jinsi Gavana wa Kirumi, au liwali Pontio Pilato, alivyojiunga na Viongozi wengine kupotosha ukweli wa kufufuka kwa Yesu, na kusema kwamba wanafunzi wake waliuiba mwili wake, wakati askari walinzi walipokuwa wamelala, na kuwadanganya watu, ingawa wao wenyewe waliujua ukweli.
"Pilato aliwadanganya watu hao kwa muda tu, lakini hatimaye ukweli ulikuwa dhahiri, walipomwona Yesu kati yao kwa muda wa siku 40. Unaweza kuwadanganya watu kwa muda tu, lakini hatimaye ukweli hudhihirika, na kumfedhehesha yule aliyeupotosha ukweli huo", alisema.
Aliendelea kusema kuwa, hata leo kuna upotoshaji wa kweli mbalimbali za kiroho na kimwili. Baada ya kuelezea juu ya baadhi ya kweli za kiroho zilizopotoshwa, aliwageukia wanasiasa waongo, akianza kwa kutoa mfano wa Waziri wa Habari wa Iraq, wakati wa vita ya mwaka 2003, Muhammad Saeed al-Sahhaf, aliyekuwa akipotosha ukweli kuhusu jinsi Iraq ilivyokuwa inapigwa vibaya katika vita hivyo, na akaendelea kusema;
"Kabla sijaendelea, nifafanue kwanza juu ya watu wanaopotosha ukweli, kwa kusema kwamba eti Wachungaji hawapaswi kuwakemea wanasiasa wananapopotoka. Watu hawa hawajui Biblia. Katika MAMBO YA WALAWI 4:22-23, Biblia inasema, Mtawala akifanya dhambi, inampasa Kuhani yaani Mchungaji, kumjulisha dhambi yake."
Kakobe aliendelea kusema kwamba huu ni mwaka wa Uchaguzi, hivyo Watanzania wawe makini na wanasiasa waongo wanaofanya uongo kuwa sehemu ya siasa zao.
"Siasa, ni Sayansi, inaitwa POLITICAL SCIENCE, na "any kind of science only deals with facts". Wanasiasa hawana budi kuwa wakweli kwa kuwa siasa ni sayansi.
"Siasa siyo mchezo mchafu, bali baadhi ya wanasiasa ndiyo wachafu. Msidanganywe tena na wanasiasa ambao watakuja kwenu mwaka huu na ahadi za uongo za kuibadili miji na kuifanya kuwa kama New York, kwa miaka mitano; na wengine hawana AIBU, wanaweza hata kuwaambia wakazi wa Dodoma kwamba watawaletea meli! Hamna budi kuyachunguza kwa makini maneno yao, na kuona kama ni ya kweli."
Kuhusu Katiba, Kakobe aliwaunga mkono Maaskofu waliowapa Wakristo maelekezo ya kuikataa Katiba Pendekezwa, katika Kura ya Maoni, na kusema kwamba hiyo ndiyo kazi ya Mchungaji.
"Mchungaji, pia ni Mwalimu, kazi yake ni kuchunga na pia kulisha kondoo (YOHANA 21:15-17), na Biblia inafafanua juu ya kazi ya Mwalimu katika ISAYA 30:20-21, ikieleza kwamba Mwalimu anatakiwa kuwaambia anaowaongoza, "Njia ni hii ifuateni, wageukapo kwenda kulia au kushoto".
Aliendelea kusema, "Kumekuwa na udanganyifu au upotoshaji wa ukweli kuhusu Katiba, tangu katika hatua za mwanzo kabisa za mchakato wa Katiba, ambapo Chama kimoja cha siasa, kiliwapachika makada wake katika vikundi mbalimbali, ili kiwe na wajumbe wengi.
"Kwa mfano Kingunge Ngombale Mwiru aliwawakilisha waganga wa kienyeji, lakini cha ajabu, ukienda kwake hata leo, hakuna kibao kwake kinachozitambulisha kazi zake za uganga wa kienyeji, kama ilivyo kwa waganga wengine! Siyo hilo tu, kote duniani, Katiba yoyote ya nchi, lazima itokane na muafaka wa Kitaifa, ili Katiba hiyo iwe na sifa ya kusomeka katika Utangulizi wake, "SISI WANANCHI".
"Hapa kwetu, watawala hawakutaka kabisa muafaka katika kutengeneza Katiba yetu, lakini wanadai eti, Katiba Pendekezwa, ni bora kuliko zote Afrika! Huu ni upotoshaji wa ukweli, wa hali ya juu sana."
Aliendelea kusema kwamba, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni, hazikuzingatiwa kikamilifu katika mchakato huo uliojaa udanganyifu.
"Sheria ya Kura ya Maoni, Ibara ya 5(3), inasema kwamba kungetakiwa kuwepo na elimu kwa wapiga kura, kwa siku 60, mara tu baada ya Tangazo la Katiba Pendekezwa katika Gazeti la Serikali Na. 382 lililotolewa tarehe 10.10.2014, lakini elimu hiyo iliyopaswa kutolewa na Tume ya Uchaguzi, haijafanyika hadi hivi leo!
V"ilevile, Sheria ya Kura ya Maoni Ibara ya 4(3) na 4(4), inasema kwamba kungetakiwa kutangazwa katika Gazeti la Serikali, SWALI LA KURA YA MAONI, ambalo wananchi wangelijibu kwa jibu la NDIYO au HAPANA, na pia Sheria ya Kura ya Maoni Ibara ya 12(1) na 12(2) na Ibara ya 16(1) inasema kwamba, kungetakiwa kuwepo na Kamati mbili za Kura ya Maoni, Kamati moja ya NDIYO, na nyingine ya HAPANA, ambazo zingejumuisha wananchi wenye misimamo tofauti kutoka katika makundi mbalimbali katika jamii, na Kamati hizo zingepiga kampeni kwa siku 30.
"Yote haya hayakuzingatiwa, lakini kinyume chake, Watawala hadi hivi leo, hawataki hata kusikia watu wakisema HAPANA kwa Kura ya Maoni, na wakati huohuo, wengine bado wanataka Kura ya Maoni ifanyike Aprili 30, pamoja na kwamba imetangazwa na Tume ya Uchaguzi, kwamba imeahirishwa!
"Wachungaji wengine wenye njaa, wanathubutu kusema kwamba eti kwa sababu kwenye Katiba Pendekezwa kuna Uhuru wa kuabudu, basi sisi Wachungaji tukae kimya, mengine hayatuhusu, hawa wana njaa kali, na upeo mdogo wa uelewa wa mambo haya.
"Mimi sina njaa, na ninasema kwa msisitizo, Katiba ni zaidi ya Uhuru wa kuabudu. Ilikuwa rahisi kwa Pilato kuwadanganya watu wa nyakati hizo, lakini leo ni kazi sana kuwadanganya watu wanaopata maarifa na habari juu ya yote yanayofanyika kote duniani, kwa TV, Redio, Magazeti, Intaneti na Mitandao ya kijamii.
"Watu wanajua kwamba kote ulimwenguni, Katiba ya Wananchi hutokana na muafaka, na Kura ya Maoni, hufanyika baada ya Kampeni ya NDIYO na HAPANA, kama ilivyofanyika Kenya ambako waliosema NDIYO waliitwa kundi la NDIZI, na waliosema HAPANA waliitwa kundi la CHUNGWA.
"Waliowaambia Wakristo wapige kura ya HAPANA kwenye Kura ya Maoni, ninawapa asilimia 90, hata hivyo kwa unyenyekevu, mimi ninaomba kuhitilafiana nao, kwa kuongeza kwamba Kura ya Maoni inapaswa kususiwa kabisa, kwa sababu kushiriki katika Kura hiyo, ni kuuhalalisha udanganyifu wa Watawala hawa, na kujifedhehesha mwishoni.
"Tangu mwanzo, watu hawa walitumia ubabe na wizi wa kura wa dhahiri katika Bunge la Katiba, na kutangaza kura feki za NDIYO za mahujaji na wajumbe wengine ambao hawakuwepo ukumbini wakati wa kupiga kura, na pia kura za Wazanzibari feki, na hivyo kupitisha kwa lazima, Katiba Pendekezwa.
"Wamedhamiria kufanya hivyohivyo hata katika Kura ya Maoni, ili kuipitisha kwa lazima Katiba yao Pendekezwa; ukizingatia kwamba, ili kutimiza kusudi hilo, wameweka sheria mbaya kwa makusudi ya kuhalalisha udanganyifu.
"Kwa mfano Sheria ya Kura ya Maoni Ibara ya 34(2), inahalalisha wapiga kura walioandikishwa Tanzania Bara, kwenda kupiga kupiga Kura ya Maoni, huko Zanzibar. Katika mazingira haya, Kura za HAPANA zitasaidia nini? Ni kuhalalisha tu udanganyifu wao, na kujifedhehesha.
"Mwandishi Mkuu wa Katiba Pendekezwa, yeye mwenyewe amesema anapenda aitwe JOKA LA MAKENGEZA! Niliposikia juu ya Jina lake hili, nilipigwa na butwaa!
Katika Biblia, Joka ni Ibilisi au Shetani (UFUNUO 12:7-9; 20:1-2), maana yake ni kwamba Mwandishi Mkuu wa Katiba Pendekezwa, ni Joka yaani Shetani, na hivyo tunaweza kusema Katiba hiyo ni ya Kishetani, maana imetokana na Shetani ambaye ni Joka lililoko kuzimu!
"Kumbe basi, siyo tu kwamba Katiba Pendekezwa imeahirishwa, ila ni kwamba Mungu ameikataa tangu siku ya kwanza ya mchakato wake!
"Kwa sasa tuwaze tu kujiandikisha kwa wingi katika Uandikishaji wa Wapiga Kura, kwa BVR, na kuwa tayari tu kwa Uchaguzi Mkuu, na kuisahau kabisa Kura ya Maoni."
0 comments:
Post a Comment