2014-12-21

Kauli chafu alizowahi kuzisema aliyekuwa mwanasheria Mkuu wa serikali Werema kuhusu IPTL/ ESCROW



MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, alishinikiza kampuni ya Independent Power Tanzania (IPTL) ilipwe fedha zilizokuwepo katika akaunti ya Escrow kiasi cha kufananisha wanaopinga hilo na ‘mawakili wa shetani,’ imefahamika. 



Habari hizi zimeibuka katika kipindi ambacho Bunge la Tanzania linaanza rasmi kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu namna fedha hizo, kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 200, zilivyochotwa kutoka katika akaunti hiyo. 


Raia Mwema sasa linafahamu kwamba kwa kutumia wadhifa wake, Werema alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, Oktoba mwaka jana, akimtaka akubali IPTL, ambayo tayari ilikuwa inamilikiwa na kampuni ya Pan African Power (PAP), ilipwe fedha za Escrow haraka. 


Katika barua yake hiyo yenye Kumb. Na AGCC/E.80/6/65 ya Oktoba 2 mwaka huu ambayo Raia Mwema limefanikiwa kuona nakala yake, Werema alimwambia Likwelile kwamba hakutakuwa na tatizo lolote kama IPTL watapewa fedha za Escrow. 
“Uamuzi wowote wa kutoa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow hauna tatizo, unalindwa kisheria na umezibwa na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia hukumu ya Jaji John Utamwa. 
“Uamuzi huu wa Mahakama Kuu umetupa sasa fursa ya kuhakikisha suala hili la IPTL linamalizika. Hii ni bahati ya mtende kwetu kumaliza suala hili. Tunatakiwa kuchukua hatua sasa badala ya kuwa mawakili wa shetani,” aliandika Werema. 


Werema aliingia katika matatizo ndani ya Bunge kutokana na majibizano yake na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, kiasi cha kufikia hatua ya kumuita mbunge huyo tumbili na yeye mwenyewe kuitwa mwizi. 


Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi ndiyo viongozi wanaotajwa kusaidia kufanikisha kutolewa kwa fedha hizo kutoka kwenye akaunti hiyo. 
Ni Werema na Maswi ndiyo waliokuwa vinara wa mashambulizi dhidi ya wabunge waliokuwa mstari wa mbele kutaka suala hilo lichunguzwe, na Katibu Mkuu huyo aliwahi kuita ushahidi wa wabunge kuwa unatokana na karatasi za kupikia maandazi. 


Kwa mujibu wa taarifa za awali kutokana na uchunguzi uliofanywa na CAG, fedha zilizokuwamo katika akaunti ya Escrow zilipaswa kulipwa kwa Tanesco kama malipo ya kutozwa kiwango kikubwa cha huduma za kutumia mitambo ya IPTL kuzalisha umeme.

Raiamwema

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...