2014-12-31

mapema; Hakimu ajitoa kesi ya kina Sheikh Farid,

Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) visiwani Zanzibar, Sheikh Farid Ahmed
Hakimu Mkazi wa Mahakama Kisutu jijini Dar es Salaam, Hellen Riwa, amejitoa kusikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) visiwani Zanzibar, Sheikh Farid Ahmed na wenzake 21.


Hakimu Riwa amechukua hatua hiyo wakati upande wa washtakiwa ukiitaka mahakama imbadilishe kwa kutokuwa na imani naye.

Oktoba 1, mwaka huu, Hakimu Riwa alitoa uamuzi juu ya maombi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi ambayo ni pamoja na kufutwa kwa kesi hiyo kwa madai kuwa hati ya mashtaka ilikuwa haifafanui maeneo wanakodaiwa washtakiwa hao kujihusisha na ugaidi na Mkurugenzi wa Mashtaka kushindwa kueleza mashtaka yanawakabili washtakiwa hao.

Akitoa uamuzi wa kujiondoa katika kesi hiyo jana, Hakimu Riwa, alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kujibu maombi hayo ya upande wa utetezi yaliyowasilishwa Septemba 19, mwaka huu na Jaji Dk. Fauz Twaib wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.


Katika ombi hilo, upande huo ulimtaka hakimu huyo kutoa uamuzi kuhusu maombi yake dhidi ya wateja wake hao.

Upande huo, ukiongozwa na Wakili, Abubakar Salim akisiadiwa na Abdallah Juma, Ubaidu Hamidu na Abdul Fatah Abdallah, uliiomba mahakama hiyo ibadilishe hakimu mwingine wa kuisikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa Hakimu Liwa aliamuru irudishwe Mahakama Kuu.

Nalo Jopo la Mawakili wa Serikali likiongozwa na Wakili Mwandamizi Mkuu wa Serikali, Benard Kongola, Peter Njike na George Barasa, lilidai kuwa ombi hilo halina msingi kwa kuwa Mahakama Kuu iliaagiza uamuzi utolewe na Mahakama ya Kisutu lasivyo, wakiendelea kufanya hivyo watamaliza mahakimu wote.

Hakimu Riwa alisisitiza kuwa hawezi kutoa uamuzi juu ya maombi hayo ya upande wa utetezi huku akisisitiza Januari 13, mwakani kesi hiyo itatajwa mbele ya hakimu mwingine atakayepangwa kuisikiliza.

Katika shtaka la kwanza, inadaiwa kuwa washtakiwa hao kati ya Januari 2013 na Juni mwaka huu katika maeneo ya ndani ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, walikula njama na kuingiza watu nchini kushiriki vitendo vya kigaidi.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa kuwaingiza watu hao nchini kushiriki vitendo vya ugaidi huku wakijua ni kosa kisheria.

Vilevile shtaka la tatu, washtakiwa Farid na Mselem, wanadaiwa kuwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014 katika maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliwaajiri Sadick Absaloum na Farah Omary kushiriki katika kutenda vitendo hivyo vya kigaidi.

Kwa upande wa shtaka la nne, mshtakiwa Farid, anadaiwa kuhifadhi watu waliotenda vitendo vya kigaidi huku akijua ni kosa kwa mujibu wa sheria.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Jamal Swalehe, Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah Hassan, Hussein Ally, Juma Juma.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...