Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepangua ratiba ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ili kuziwezesha timu nne kushiriki Kombe la Mapinduzi linalotarajiwa kuanza kesho kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Tanzania Bara itawakilishwa na Yanga, Simba, Azam FC na Mtibwa Sugar katika mashindano hayo ya maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura alisema jana kuwa kutokana na timu hizo kushiriki katika mashindano hayo, mechi zao za raundi ya tisa na 10 ya Ligi Kuu zitachezwa baada ya timu hizo kumaliza michuano hiyo.
Wambura alisema mechi za ligi ambazo hazitachezwa wiki hii ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar, Mbeya City na Yanga, na ile kati ya Mgambo Shooting na Simba. Mechi za wiki ijayo zinazopisha michuano hiyo ni kati ya Kagera Sugar na Azam, Coastal Union na Yanga, Mbeya City na Simba na ile ya Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Mapinduzi, Sherry Khamis alisema timu zote zitakapokuwa visiwani na hapo ndipo ratiba kamili ya mashindano hayo itakapotolewa.
Khamis alisema kutokana na taratibu ngumu walizopewa na timu za nje, mwaka huu mashindano hayo yatashirikisha timu moja tu kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.
“Mabingwa watetezi tu KCCA ya Uganda ndiyo itashiriki, tulikuwa na maongezi na timu ya Ulinzi ya Kenya, hata hivyo hatukuweza kufikia mwafaka kutokana na masharti magumu,” alisema Khamis.
Alizitaja timu nyingine kuwa ni KMKM, JKU, Mafunzo, Mtende na Shaba FC. Alisema ratiba yao itakuwa na mechi mbili kwa siku yaani jioni na usiku.
Mshindi wa kwanza atazawadiwa kitita cha Sh10 milioni na wa pili Sh5 milioni, pia kutakuwa na zawadi za mfungaji bora na kipa bora.
0 comments:
Post a Comment