Hatimaye kampeni ya Nani Mtani Jembe iliyodumu kwa takribani miezi miwili ilihitimishwa kwa pambano kali lililowakutanisha miamba wa soka nchini klabu za Simba na Yanga.
Mchezo huo uliotanguliwa na tambo pamoja na majigambo wiki mbili kabla ulifanyika hiyo jana huku mashabiki wa timu zote wakiwa na uhakika kuwa timu yao ndio ingeibuka na ushindi.
Pambano hilo lilichezeshwa na mwamuzi wa Jonesia Rukyaa toka Bukoba ambaye kwa kiasi kikubwa aliweza kulimudu kwa dakika zote 90 za mchezo.
Katika mchezo huo wekundu wa Msimbazi Simba walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa bila ambayo yote yalitiwa kimiani kipindi cha kwanza kupitia kwa Awadh Juma ambaye katika dakika ya 30 aliupokea mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Emmanuel Okwi na kuukwamisha wavuni. Katika dakika ya 42 Yanga walijikuta wakiruhusu bao la pili baada ya Elias Maguri kuumalizia mpira uliogonga mwamba kufuatia kichwa cha Simon Serunkuma na kufanya timu hizo ziende mapumziko Simba ikiwa kifua mbele.
Kipindi cha pili Yanga walionekana kuutawala zaidi mchezo huku mabadiliko ya kumuingiza Mrisho Ngassa yakionekana kuwaongezea nguvu lakini hata hivyo safu ya ulinzi ya Simba ilisimama imara na kutoruhusu bao zaidi.
Shamrashamra wakati wa mapumziko
Mashabiki wa Simba wakiwa wamebeba mfano wa jeneza kama ishara ya kuwakejeli watani wao wa jadi baada ya kushinda
0 comments:
Post a Comment