2014-12-31

Nishida;Lundenga alia hujuma

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kuifungia Kampuni ya Lino International kuendesha mashindano ya Miss Tanzania kwa miaka miwili, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Hashim Lundenga amesema hatua hiyo imefikiwa kutokana na shinikizo kutoka kwa baadhi ya watu wenye dhamira ya kuitoa kwenye mstari wa mafanikio sanaa ya urembo nchini. 



Lundenga alisema jana uamuzi wa Basata ni utekelezaji wa dhamira ya wachache walioamua kuhakikisha Miss Tanzania inapotea kwenye ramani ya burudani nchini.


Lundenga alisema uamuzi huo wa upande mmoja, haujaangalia mafanikio ya mashindano hayo kwa miaka 21 tangu kuanza kwake na wala hatima yake baadaye.


“Niseme kweli, kwa mtu mwenye mapenzi ya kuona sanaa ya urembo inasonga mbele kwa mafanikio, kamwe hawezi kuchukua uamuzi wa kukomoa kama huu, ila kwa watu wachache walioamua kuharibu taswira ya mashindano kwa sababu zisizo na uzito, wanaweza kufanya hivyo,” alisema Lundenga.


Aliongeza: “Siko hapa kutaja majina ya watu waliojipanga kuharibu mashindano haya, lakini kwa akili isiyohitaji kazi kubwa kufikiria jambo rahisi kama hili, haiwezi kupata tabu kuamini ukweli kwamba kuna watu nyuma ya uamuzi huu wa Basata.” 



Lundenga alisema wameshangazwa na uamuzi huo wa kufungiwa, kwani umekuja katika mazingira yasiyoeleweka ambayo hayakuwapa fursa ya kujieleza.


“Tumefanya mashindano haya kwa mafanikio kwa miaka zaidi ya 20, iweje leo tunapewa adhabu kubwa kiasi hicho kwa makosa madogo,” aliongeza Lundenga.


Akifafanua, Lundenga alisema Novemba 21 mwaka huu, walipewa barua ya onyo yenye vipengele vinne na kutakiwa kuvishughulikia kwa ajili ya msimu wa mwakani, lakini Desemba 22 mwaka huu walipewa barua ya kutakiwa kusimamisha mashindano.


“Kuna tatizo hapa. Leo unapewa barua ya onyo kabla hujafanya chochote unapewa barua ya kusimamishwa tena bila hata kupewa nafasi ya kujitetea. Ni aina gani ya uamuzi kama si kuwa na watu wenye nia mbaya na mashindano haya,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...