2014-12-17

TANZANIA - ZAMBIA - KENYA ZASAINI MAKUBALIANO YA USAFIRISAJI UMEME

Waziri wa Nishati na Madini nchini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), Waziri wa Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji wa Zambia, Christopher Yaluma (katikati), na Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Davis Chirchir (kulia) wakisaini Makubaliano ya Awali (MoU) ya mradi wa pamoja wa kujenga miundombinu ya kusafirisha umeme kati ya nchi za Zambia, Tanzania na Kenya.… 


Waziri wa Nishati na Madini nchini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), Waziri wa Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji wa Zambia, Christopher Yaluma (katikati), na Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Davis Chirchir (kulia) wakisaini Makubaliano ya Awali (MoU) ya mradi wa pamoja wa kujenga miundombinu ya kusafirisha umeme kati ya nchi za Zambia, Tanzania na Kenya. 

Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Davis Chirchir (aliyesimama) akizungumza wakati wa hafla iliyofanyika nchini Zambia ya kutiliana saini Makubaliano ya Awali (MoU) ya mradi wa pamoja wa kujenga miundombinu ya kusafirisha umeme kati ya nchi za Zambia, Tanzania na Kenya. Wengine katika picha ni Waziri wa Nishati na Madini nchini, Profesa Sospeter Muhongo (wa tatu kushoto), Waziri wa Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji wa Zambia, Christopher Yaluma (wa nne kushoto), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini nchini, Eng.Ngosi Mwihava, (wa kwanza kushoto), pamoja na watendaji wengine kutoka nchini Kenya, Zambia na Umoja wa Ulaya.
                                                

Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme nchini (Tanesco), (mstari wa mbele) waliohudhuria hafla iliyofanyika nchini Zambia ya kutiliana saini Makubaliano ya Awali (MoU) ya mradi wa pamoja wa kujenga miundombinu ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kati ya nchi za Zambia, Tanzania na Kenya wakimsikiliza mmoja wa wazungumzaji katika hafla hiyo (haonekani pichani).
 Kutoka kulia ni Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli, Eng. Hosea Mbise, Decklan Mhaiki, Naibu Mkurugenzi Mtendaji-Uwekezaji (Tanesco), Kasindi Malale, Injinia Mkuu (Tanesco), Leonard Masanja, Injinia Mkuu (Wizara) na Mwanasheria, Abbas Kisuju (Wizara).


Nchi za Tanzania, Zambia na Kenya zimetiliana saini Makubaliano ya Awali (MoU) ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa miundombinu ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa kilovolti 400.
 Makubaliano hayo ya awali yamesainiwa tarehe 15 desemba 2014, nchini Zambia na Mawaziri wanaosimamia sekta ya Nishati katika nchi husika ambao ni Waziri wa Nishati na Madini nchini, Profesa Sospeter Muhongo,Waziri wa Wizara ya Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji wa Zambia,Christopher Yaluma, na Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Davis Chirchir.


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameeleza kuwa kukamilika mwa mradi huo kutaziwezesha nchi hizo kuuziana umeme wa bei nafuu ambao utakuwa chini ya senti 10 za Kimarekani kwa uniti moja .“ Mradi huu utakamilika kwa awamu kati ya mwaka 2016 na 2018. 

Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia juhudi za serikali za kuachana na mitambo ya dharura ambayo inauza umeme huo kwa gharama ya kati ya senti 30 na 55 za Kimarekani kwa uniti moja”, alisema Profesa Muhongo. 
                                      


Profesa Muhongo aliongeza kuwa Tanzania inahitaji umeme mwingi, wa bei nafuu na wa uhakika ili kuongeza uzalishaji, uwekezaji, ushindani,kutengeneza ajira mpya na kukuza uchumi imara. 

Mradi huo utakuwa na manufaa mbalimbali kwa nchi husika ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa nchi hizo, kutumia rasilimali umeme kwa ufanisi zaidi, kutoa fursa kwa nchi wanachama kuweza kufanya biashara ya kuuziana umeme na kupanua upatikanaji wa umeme kwa wananchi husika.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...