“Sitasahau siku niliyokimbiwa na mume wangu baada ya kumzalia pacha kwa mara ya tatu mfululizo.” Hii ni kauli ya Salome Paul Mhando, mama wa watoto sita ambao ni pacha, aliowazaa kwa nyakati tofauti katika kipindi cha miaka sita iliyopita, wakipishana miaka miwili miwili.
Salome, alitelekezwa nyumbani na mumewe huyo baada ya kujifungua pacha kwa mara ya tatu, huku wakiwa hawana sehemu maalumu ya kuishi, achilia mbali njaa iliyotokana na umaskini wa kipato.
Baada ya kutelekezwa, msamaria mwema alijitolea kumhifadhi katika shamba lake lililopo eneo la Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kabla ya kupata msaada wa nyumba ya kuishi.
Mama huyo anayekumbuka tukio hilo kwa uchungu, anasimulia kuwa mumewe aliyemtaja kwa jina moja la Ali, alimtoroka saa saba mchana na kumwacha akiwa na pacha hao.
Anabainisha kuwa tukio hilo lilitokea baada ya familia hiyo kukaa na njaa kwa siku kadhaa kutokana na umaskini wa kipato.
“Siku hiyo, ambayo tarehe yake siikumbuki, mume wangu alirudi nyumbani akiwa tena hana chakula na kunieleza kuwa anaumwa. Nilipomwuuliza sasa tunafanyaje kuhusu chakula, alitoka nje,” anaeleza mama huyo na kuendelea:
“Nikaamua kumfuata na kuanza kumsema nikimdai chakula. Baadaye (mumewe) akaniuliza mbona unanisema? Mimi nikamjibu; naulizia masuala ya chakula, tunafanyaje leo? Akasema; basi niache naenda kukitafuta.”
Salome anaeleza kuwa kinyume na ahadi hiyo, tangu wakati huo alipoondoka hajaonekana nyumbani hadi sasa. “Niliamua kwenda kulala, lakini nikiwa na wasiwasi kuhusu usalama wake. Nikapatwa na hofu nikijiuliza; nini kimempata mwenzangu na kuanza kuwapigia simu ndugu zake ambao pia hawakupatikana.”
Salome anasema jitihada za kuwatafuta ndugu wa mumewe ziligonga mwamba na hadi sasa hana mawasiliano yoyote na familia hiyo ya mumewe.
Anaeleza kuwa kutokana na mumewe huyo kutorudi tena nyumbani, alilazimika kwenda kwenye vyombo vya habari kuomba msaada wa malezi ya watoto hao.
“Nilikwenda kwanza ITV ambako mbali na kunisaidia katika mahitaji ya msingi ya chakula, walinitangaza pia kwenye luninga kuwa ninahitaji msaada na tukio hilo ndilo limenisaidia kupata msaada wa kudumu.
0 comments:
Post a Comment