WATU wawili wamekufa mkoani Singida katika matukio tofauti yaliyotokea hivi karibuni, likiwemo la mwanamke mmoja kupigwa na rungu na mumewe kutokana na kile kinachodhaniwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka alisema kuwa tukio la kwanza lililotokea kijiji cha Songambele, kata ya Ndago wilayani Iramba Januari 11 mwaka huu majira ya saa 1.00 asubuhi ni la mauaji ya Maria Shila (57) yaliyofanywa na mumewe Lucas Kitundu (47).
Akisimulia mkasa huo, Sedoyeka alisema kuwa kabla ya tukio hilo wana ndoa hao walikuwa na ugomvi wa mara kwa mara ambapo Kitundu alikuwa akimtuhumu mkewe Maria kutokuwa mwaminifu kwenye ndoa yao.
Alisema kuwa siku ya tukio, wanandoa hao walionekana klabu ya pombe ya kienyeji wakiwa wanalumbana na asubuhi ya siku iliyofuata mwili wa Maria uligundulika ukiwa umetelekezwa nje ya nyumba yao huku pembeni mwake kukiwa na rungu lililojaa damu.
“Aliyegundua mwili huo ni mdogo wa marehemu ambaye alikuwa na miadi ya kumpitia siku hiyo kwa ajili ya kwenda naye kanisani,” alisema Kamanda Sedoyeka.
Kamanda Kamwela alisema kuwa uchunguzi wa awali wa Polisi unaonesha kuwa Kitundu alikuwa akiishi nyumbani kwa marehemu na mara baada ya kufanya kitendo hicho alichukua vitu vyake, zikiwemo nguo, na kutoweka kusikojulikana ambapo hadi sasa hajapatikana.
Katika tukio la pili lililotokea Januari 12 mwaka huu huko katika kijiji cha Mguluwang’ombe wilayani Manyoni, mtoto Laurent Buji (5) alipoteza maisha akiwa njiani kupelekwa hospitalini kwa matibabu baada ya kutumbukia kwenye shimo la choo lililokuwa limejaa maji.
0 comments:
Post a Comment