2015-01-21

Kazi Kwao;Vigogo escrow waanza kulipa kodi ya TRA


Dar es Salaam. Baadhi ya vigogo walionufaika na mgawo wa mabilioni ya fedha kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow wameanza kulipa kodi kuanzia Januari Mosi kama ilivyoagizwa na Serikali.


Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade alisema jana kuwa vigogo hao wameanza kulipa kodi lakini hakuwa tayari kuwataja wahusika wala kiwango cha fedha kilichokusanywa licha ya kusema suala hilo linasimamiwa kwa umakini na TRA.


“Wameshaanza kulipa ila siruhusiwi kuwataja kwa majina. Wanaotakiwa kulipa ni wale waliotajwa katika ripoti,” alisema Bade.


Alisema wale ambao watashindwa kulipa kodi hiyo baada ya Januari 30, mwaka huu, watakumbana na adhabu ya kutozwa faini kulingana na sheria zilizopo.


Baadhi ya walionufaika na mgawo huo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni), aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka (Sh1.6 bilioni) na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (Sh40.4 milioni).


Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni), Mbunge mstaafu wa Sumbawanga, Paul Kimiti (Sh40.4 milioni) na aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni).


Wapo pia majaji wawili, Profesa Eudes Ruhangisa (Sh404.25 milioni) na Aloyce Mujulizi (Sh40.4 milioni).


Sakata la ufisadi wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow pia limewang’oa wafanyakazi saba wa TRA.


Wengine ambao tayari wameshawajibika katika kashfa hiyo ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema aliyejiuzulu, Profesa Tibaijuka aliyefukuzwa kazi na Rais Kikwete na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.


Meneja wa TRA apata dhamana


Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Mutabingwa anayekabiliwa na kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh1.6 bilioni kutoka akaunti ya Tegeta escrow katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana aliachiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti.


Hakimu Mkazi, Frank Moshi jana alimwachia huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...