2015-01-21

Kume Kucha;Sakata la Escrow: Ikulu Yaeleza hatima ya Kiporo cha Muhongo, Yasema Rais Kikwete atatimiza Ahadi hivi Karibuni


IKULU imewataka Watanzania kuwa na subira kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati wowote kuanzia sasa atatoa uamuzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.


Profesa Muhongo na baadhi ya viongozi wengine wa Serikali wanahusishwa na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Viongozi wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi ambaye amesimamishwa kupisha uchunguzi, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye amejiuzulu na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye tayari uteuzi wake umetenguliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alisema si kweli Rais Kikwete anakwepa kumwajibisha Profesa Muhongo kama watu wengi wanavyodai.

Alisema kinachofanywa na Rais Kikwete ni kufuata utaratibu unaotakiwa.

“Siku mbili tatu alizosema rais maana yake ni hivi karibuni na msidhani anakimbia kutoa uamuzi… siku si lazima zihesabike, ni siku yoyote atatoa majibu.

“Tena nawaambia msikomalie suala hili kama vile ni la kufa na kupona, rais atalifanyia kazi muda si mrefu,” alisema Salva.

Alisema taratibu za kumwajibisha Profesa Muhongo kama kiongozi wa kisiasa hazifanani na hatua zilizochukuliwa kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Maswi kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Serikali.

Akizungumzia ziara za Profesa Muhongo anazoendelea nazo mikoani, Rweyemamu alisema tuhuma hizo hazimzuii kufanya kazi kwa kuwa bado hajaondolewa kwenye nafasi ya uwaziri aliyonayo.

“Huyu bado ni waziri, ana haki ya kuendelea na ziara zake kama kawaida, kumbukeni wizara yake ina mambo mengi ambayo yanapaswa kusimamiwa kila siku,” alisema Rweyemamu.

Desemba 22, mwaka jana, Rais Kikwete akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema amemuweka kiporo Profesa Muhongo maana bado hajapata ufafanuzi kuhusu mambo kadha wa kadha, na kwamba baada ya siku mbili, tatu, atakapopata ufafanuzi na kujiridhisha, atachukua uamuzi.

Siku nne baadaye, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema Rais Kikwete bado hajakamilisha kulishughulikia suala hilo na kwamba litakapokuwa tayari wananchi watajulishwa hatua alizochukua.

MISAMAHA YA KODI
Kuhusu misamaha ya kodi ambayo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema imeongezeka kutoka Sh trilioni 1.48 mwaka 2012/13 hadi trilioni 1.82 mwaka 2013/14, ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 334, Rweyemamu alisema wabunge ndio wanapaswa kulalamikiwa.

Alisema katika Bunge lililopita Serikali ilipeleka muswada wa kufuta misamaha ya kodi, lakini wabunge hawakuupitisha.

Rweyemamu alisema bila kupitisha muswada huo na hatimaye uwe sheria, suala hilo halitakwisha.

“Wabunge wanapiga kelele kuhusu misamaha ya kodi wakati mwaka jana Serikali ilipeleka muswada wa kufuta misamaha waliukataa na kuuchanachana…tunawaomba siku nyingine wakipelekewa waupitishe.

“Sisi hatupendi haya mambo na kama wanaonekana hawapendi, tunawashauri waupitishe ule muswada ili tuondokane na tatizo hili,” alisema Rweyemamu

KURA YA MAONI
Katika hatua nyingine, Rweyemamu alikanusha taarifa zinazoendelea kusambazwa kuwa Rais Kikwete alivunja sheria ya kura ya maoni kutokana na kutopelekwa Katiba iliyopendekezwa kwenye Gazeti la Serikali.

“Hizi taarifa si za kweli, Rais Kikwete alitimiza taratibu zote kulingana na matakwa ya kura ya maoni, baada ya kupokea Katiba inayopendekezwa Oktoba 8, mwaka jana, ilipofika Oktoba 10, ilitangazwa katika Gazeti la Serikali,” alisema Rweyemamu.

Alisema hawana hofu kwa vile maandalizi ya kura ya maoni yanaendelea vizuri.

Rweyemamu alisema nakala za Katiba inayopendekezwa zitatolewa kwa ajili ya kutoa elimu japokuwa hazitawafikia watu wote kutokana na wingi wa wananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...