Aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samweli Sita akisalimiana na rais Jakaya Mrisho Kikwete.
MWAKA huu unaingia katika historia ya nchi yetu moja kwa moja pasipo maswali. Tofauti na wakati mwingine, mwaka huu una uwezekano wa kupitisha matukio makubwa mawili, ambayo kwa namna yoyote, yanaweza kuharibu au kuimarisha taifa letu lenye umri wa miaka 50 tangu lipate uhuru wake.
Tukio moja tumelizoea kwa sababu tunalipitia kila baada ya miaka mitano, ambalo linahusu uchaguzi mkuu wa kutupatia rais, wabunge na madiwani mpya kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Hii itakuwa ni mara ya tano kwa wananchi kujipanga vituoni kufanya uchaguzi tangu tuanze mfumo wa vyama vingi, 1992.
Ingawa tangu tuanze kufanya hivyo mara zote Chama Cha Mapinduzi kimeibuka kidedea katika nafasi ya urais, kama inavyotarajiwa tena safari hii, lakini uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na changamoto nyingi, kwani kwa mara ya kwanza, CCM inahisi upinzani wana nafasi ya kushika dola, kutokana na kuimarika kwa kambi ya upinzani na migawanyiko ya ndani kwa ndani miongoni mwa makada wake.
Ni uchaguzi unaokuja huku wapinzani wakitangaza kuungana kwa kusimamisha mgombea mmoja kwa kila nafasi, kwa kila jimbo na kata, kupitia umoja wao wa Ukawa. Katika nchi ambayo imeamua kufuata misingi ya demokrasia, ya kuwaachia wananchi kumchagua kiongozi wanayemtaka, lolote linaweza kutegemewa katika kinyang’anyiro hiki kinachotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu baada ya Rais Kikwete kumaliza muda wake.
Lakini ukiachana na tukio hili, lipo lingine ambalo kinadharia linaonekana ni dogo lakini kiuhalisia ni kubwa na muhimu kuliko hata Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Hili linahusu kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa ambayo katika kalenda, inaonyesha kuwa wananchi watapaswa kupiga kura ya kuikubali au kuikataa Aprili 30, mwaka huu.
Wote tunajua kuwa upitishwaji wa Katiba hii katika Bunge Maalum la Katiba lililokuwa likiongozwa na Mhe. Samuel Sitta haukuwa mzuri, kwa namna ile tuliyoitarajia baada ya baadhi ya wajumbe kususia mchakato wake kwa madai ambayo tunayafahamu. Sitaki kurejea nyuma, juu ya uhalali wake, kwa sababu ninajua kwa mujibu wa sheria, Katiba Inayopendekezwa ni halali.
Tatizo langu limekuwa juu ya namna mamlaka zinazohusika zinavyolichukulia jambo hili kirahisi, kiasi kwamba wanaacha mambo ya msingi bila sababu zenye hoja. Kwa mfano, tunahitaji kujua idadi ya wananchi watakaokuwa na hadhi ya kuipigia kura katiba hii, ambao haina namna wanavyoweza kupatikana pasipo uandikishaji upya kufanywa na Tume ya Uchaguzi yaani NEC.
Hadi ninapoandika makala haya, bado hakuna hatua zilizo wazi juu ya nini kinafanyika kuhusu uandikishwaji huu. Lakini achana na hilo, kuna hili la kutoa elimu kwa wananchi juu ya nini kilichomo ndani ya katiba inayoelezwa kuwa ni yao, ili waijue, wajiandae kuikataa au kuikubali. Zoezi la kutoa elimu hii, haliwezi kufanywa kwa kutoa makala magazetini, linatakiwa kufanywa ‘live’ ili watu wawe na nafasi ya kuuliza na kujibiwa maswali.
Labda mamlaka zinapaswa kutambua kuwa suala hili siyo la kulifanyia majaribio wala masihara, kwa sababu halina hati miliki ya chama chochote cha siasa. Kama kuna watu wanadanganyana kuwa Watanzania wanaburuzika, ni sawa, lakini muhimu kwao kutambua kuwa wataburuzika leo, siyo kila siku.
Elimu ni lazima itolewe ili wananchi wapige kura itakayosukumwa na dhamira ya mioyo yao, tusiwafanye wapige kura kwa laghai, kwa sababu watakapogundua kuwa watawala waliwalaghai, inaweza kutuletea matatizo kuliko kama tungeweza kuzuia jambo hili leo, tena pasipo gharama yoyote. Kama tunadhani tuna mambo mawili makubwa na muhimu, basi moja lisubiri.
Hili la Katiba Inayopendekezwa lisubiri, tufanye uchaguzi, tuwapate viongozi wetu wapya, wakae na kuanza mchakato wa kura ya maoni, kwa sababu tutakuwa na muda wa kutosha, tofauti na hili la zimamoto linaloonekana kutayarishwa kufanywa na watawala wetu. Kinga ni bora kuliko tiba!
0 comments:
Post a Comment