2015-01-23

Mambo magum;Wanasiasa Kenya wamshambulia Fatou Bensouda



Kiongozi wa Mashtaka wa Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC), Fatou Bensouda akizungumza na vyombo vya habari siku za hivi karibuni. Picha na Maktaba


Nairobi, Kenya. Wanasiasa waliotajwa na kiongozi wa mashtaka wa Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC), Fatou Bensouda kuhusu kesi ya Rais Uhuru Kenyatta, wamejitokeza na mmoja wao amesema upande wa mashtaka ulimtaka atoe ushahidi wa uongo.


Aliyekuwa mbunge wa Nakuru Mjini, David Manyara alisema mahakama hiyo ilimtaka awe shahidi wa upande wa ICC, lakini alikataa.


“Bensouda ananitaja kwa ubaya kwa kuwa nilikataa kuwa shahidi wa upande wa mashtaka, ingawa walitaka kunilipa Sh200 milioni ili nitoe ushahidi wa uongo kwenye kesi ya rais.


“Wanasema nilikuwa nikisambaza bunduki, wakijua sijawahi hata kugusa bunduki maishani mwangu. Mimi ni bondia na mikono yangu ndiyo silaha yangu,” alifafanua.


Mfanyabiashara Bildad Kagai alisema inasikitisha kuwa Bensouda kumhusisha na madai ya rushwa ya mwaka 2009.


“Haiwezekani kwamba ningemhonga mtu mwaka 2009, miaka mitatu kabla ya kesi ya ICC kujulikana,’’alisema.


Alisema shahidi aliyetajwa kuwa James Kabutu alikuwa rafiki yake tangu mwaka 2009 na kwamba hakuwa na haja ya kumsumbua.


Naye Mwenyekiti wa Nacada, ambaye alikuwa mbunge wa Naivasha wakati zikitokea vurugu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007, John Mututho alisema Bensouda anataka kumfurahisha mtangulizi wake Luis Moreno Ocampo.


“Ocampo anajua kwamba hakuwahi kumhoji John Mututho wala aliyekuwa OCPD wa Naivasha, Willy Lugusa. Unawezaje kufanya uchunguzi katika kesi ya kiwango cha juu namna hii bila ya kuwahoji watu waliokuwapo? Hii siyo kanuni katika kesi za uhalifu, anapaswa kuwahoji waliopo,” alihoji Mututho.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...