Dodoma. Usemi wa wahenga kuwa dalili ya mvua ni mawingu, una mashiko na huonekana kufaa kwa watu wanaojiandaa kwa jambo fulani lililo mbele yao.
Katika maandalizi ya mtu aliyedhamiria jambo huwa si rahisi kukata tamaa hata kama atakumbwa na dhoruba za aina yoyote lakini bado atahitaji kusonga mbele pasi kurudi nyuma.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo wasomi wengi wamekuwa wakikimbilia katika siasa na kuziacha taaluma zao. Pengine ni kutokana na kufuata masilahi na urahisi wa utendaji kazi.
Mbali na vijana, wapo wanaokimbia wakiwa kazini na kuingia katika siasa. Miaka ya karibuni harakati zimekuwa zikianzia vyuoni na baadhi ya walioshinda kwenye siasa tunashuhudia hadi sasa wakiwa na nyadhifa mbalimbali Serikalini; wakiwemo mawaziri.
Mary Chacha (23) ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha St. John’s cha mjini Dodoma. Ni miongoni mwa wasichana wenye ndoto ya kuwa wanasiasa wakubwa katika nchi.
Chacha anasoma Kitivo cha Elimu chuoni hapo ambaye mbali na kuwaza kwenda kufundisha katika shule za vijijini; wanakoishi watu wengi wa kipato cha chini, anatamani kupata nafasi ya uwakilishi wa kisiasa hasa katika kofia ya ubunge ili awasemee watu wa vijijini.
Katika mazungumzo na Chacha ambaye hivi karibuni alikuwa kinara wa uongozi kwa Bunge la Vijana, anasema kuwa ndoto ya kuwa kiongozi alianza kuiwaza tangu akiwa shule ya msingi.
Bunge la Vijana liliandaliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuibua vipaji na kutoa fursa kwa vijana, lilifanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa na Chacha aliteuliwa na uongozi kushika nafasi ya Katibu. Bunge hilo lililosheheni vijana wa vyuo vikuu nchini. Yafuatayo ni mahojiano na Chacha:
Hongera kwa kazi uliyoifanya ndani ya siku tatu mfululizo. Hebu tupe siri ya mafanikio yako katika kazi hii?
Jibu: Nashukuru kwa pongezi lakini nafasi hii ni kwa neema ya Mungu ndiyo nimeweza kuliunganisha Bunge hili ambalo kwa kweli ni gumu na lina changamoto nyingi za vijana.
Wakati unakuja katika bunge hili ulijua kwamba ungekuwa kiongozi au ilitokea baada ya kufika hapa ukumbuni?
Jibu. Ukweli nilikuja mimi kama mimi tena sikujua kabisa kama nitakuwa hata na nafasi yoyote ingawa nilikuja nikiamini nimejiandaa vya kutosha kwa ajili ya kuwa mmoja wa wachangiaji wazuri.
0 comments:
Post a Comment