2015-01-21

Ni balaa:Wingu zito Kura ya Maoni ya Katiba



                                  Tundu Lisu

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika amewasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu udhaifu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili ijadiliwe na kutoa maazimio kutokana na kutokuwapo uwezekano wa kufanyika kura ya maoni Aprili 30.

Dar es Salaam. Mchakato wa Katiba Mpya, hatua ya Kura ya Maoni umegubikwa na wingu zito kutokana na kuibuka utata na ukiukwaji wa sheria.

Wakati hali ikiwa hivyo, jana Ofisi ya Rais, Ikulu iliibuka na kutoa ufafanuzi kuwa Rais Jakaya Kikwete hajakiuka Sheria ya Kura ya Maoni kama ilivyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni. 


Juzi, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema kuna mwingiliano unaoleta mkanganyiko katika mchakato wa kuboresha Daftari la Wapigakura na Sheria ya Kura ya Maoni.

Jaji Warioba alisema sheria inaweka utaratibu maalumu wa mchakato wa kura ya maoni ambao hautaendana na ratiba ya uandikishwaji katika daftari hilo.

Alisema Sheria Kura ya Maoni Na. 3 ya mwaka 2014 inasema wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya kura ya maoni kwa miezi miwili na mwezi mmoja wa kampeni lakini hadi sasa, hakuna ratiba inayoeleweka, jambo ambalo alisema linaleta mwingiliano.

“Hii ni Januari, kama watafuata sheria na kuanza kutoa elimu kwa kipindi cha miezi miwili, ina maana itakuwa ni Aprili na Mei, ukijumlisha mwezi mmoja wa kampeni ambao ni Juni ina maana kura itapigwa Julai. Ikumbukwe kuwa mwezi huo mbio za uchaguzi zitakuwa zimepamba moto,” alisema.

Mkanganyiko huo umeibua maswali kutoka kwa wanasiasa, wanasheria na wanaharakati wakisema hali hiyo inaweza kuathiri kura ya maoni ambayo imepangwa kufanyika Aprili 30.

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika amewasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu udhaifu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili ijadiliwe na kutoa maazimio kutokana na kutokuwapo uwezekano wa kufanyika kura ya maoni Aprili 30. 


Kauli ya Ikulu

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu alisema katika mchakato huo, Rais Kikwete alifuata taratibu zote zilizopo katika sheria hiyo, ikiwa ni pamoja na kutangaza katika Gazeti la Serikali tarehe ya kuanza kwa upigaji wa kura hiyo.

“Sheria inasema Rais atatangaza tarehe hiyo wiki mbili baada ya kupokea Katiba Inayopendekezwa na alitekeleza hilo na baadaye alieleza jinsi ambavyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itakavyosimamia suala hilo,” alisema.

Katika hotuba yake kwa wazee wa Dodoma Novemba mwaka jana, Rais Kikwete alisema, “Ninaomba Watanzania wenzangu tuzingatie mamlaka ya Sheria ya Kura ya Maoni ambayo imeelekeza vizuri lini kura ya maoni itapigwa, lini kampeni zitafanyika na lini wadau watatoa elimu, naomba tuwe na subira. Tukizingatia sheria hii hakuna ugomvi,” alisema Rais Kikwete.



 Mwananchi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...