2015-01-14

Ni kitimtim:Watafukuzwa mawaziri wote bila kupata tiba

 Baraza Jipya La Mawaziri 2014
Mawaziri hawa ni Nizar Karamagi, Dk Ibrahim Msabaha, William Ngeleja na sasa Profesa Sospeter Muhongo ambaye kwa sasa amewekwa kiporo kwa kashfa ya Escrow.

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu, tangu mwaka 2000 na 2010, nilipata bahati ya kuhudhuria baadhi ya mikutano ya kampeni za wagombea wa urais karibu wa vyama vyote.

Katika mikutano hiyo ya kampeni, miongoni mwa mambo, waliyokuwa wanasema hasa wapinzani ni kuwa, Tanzania chini ya mfumo wa sasa, hata kama Rais wa Marekani wakati huo, Bill Clinton akiwa Rais wa Tanzania hawezi kuibadili kitu.

Kauli hii, wengi hatukuielewa lakini jambo moja ambalo lilifafanuliwa ni kuwa Tanzania ina tatizo la mfumo wa uongozi na hivyo yanahitajika mabadiliko makubwa. Mwanasiasa mmoja maarufu alitueleza kuwa ili nchi hii iweze kuwa na maendeleo mazuri, inahitaji mabadiliko ya kimfumo.

Akasema tuna matatizo lakini viongozi hawataki kubadilika. Mfano mtu ameteuliwa kuwa kiongozi kila siku anakwenda ofisini na kurudi nyumbani hana ajenda.
 
 Mwanasiasa huyu, akasema kiongozi huyu wa serikali kila siku anategemea kufanya kazi kutokana na matukio, akipigiwa siku kuna vurugu sehemu fulani anakwenda kusuluhisha, kisha anarudi ofisini bila kufikiri ajenda ya kumaliza vurugu.

Kauli za wanasiasa hao naamini zina ukweli fulani katika kupata mwarobaini wa matatizo ya Taifa letu ambalo mengi tulipaswa leo yawe ni historia.
Miaka zaidi ya 40 iliyopita, Baba wa Taifa, hayati MwalimuJulius Nyerere alisema nchi ikitaka kuwa na maendeleo inapaswa kuwa na ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora.
 Wapo mawaziri ambao wameondolewa hadi sasa “wanalia” hawajui makosa yao, lakini walibanwa wawajibike kutokana na kuziongoza wizara ambazo kuna watendaji wa chini wanafanya makosa.

Katika wizara moja tu ya Nishati na Madini kuna orodha ndefu ya mawaziri ambao wameondolewa kwa aibu. Katika Serikali ya awamu ya nne pekee mawaziri wanne wamepitia wizara hii na kuingia matatani.

Mawaziri hawa ni Nizar Karamagi, Dk Ibrahim Msabaha, William Ngeleja na sasa Profesa Sospeter Muhongo ambaye kwa sasa amewekwa kiporo kwa kashfa ya Escrow.

Hata hivyo, katika kashfa zote ambazo zimekuwa zikiwakabili mawaziri hawa kumekuwapo na utata wa kuhusika kwao moja kwa moja kijinai.
 Nadhani wizara hii moja inatosha kutufikirisha tuna tatizo gani? Ukijiuliza swali hilo, unaweza kupata miongoni mwa majibu ni mfumo wa uongozi wetu.
 Haiwezekani kufanyika ufisadi na kuchotwa zaidi ya Sh300 bilioni katika mazingira tata, wakati Taifa lina vyombo vingi vya usalama. Hapa ndipo unanipa jibu kuwa ni kweli hata kama Clinton angepewa wizara hii angefukuzwa.

Wizara kama hii moja tu, waziri huyo, amezungukwa na washauri wanaotambulika kisheria.
 Hawa ni kama vile katibu mkuu, manaibu makatibu wakuu, wakurugenzi wa bodi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wakurugenzi wa idara mbalimbali.
 Mfumo huu, ndio naamini uliisukuma hata iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba, kutoa mapendekezo juu ya kupunguzwa mamlaka ya Rais, ikiwapo uteuzi wa nafasi mbali mbali .
 Rais kwa sasa anateua mawaziri wakuu wa mkoa na wilaya, wenyeviti wa bodi, wakurugenzi wa mashirika ya umma na wenyeviti wa bodi, majaji, wakuu wa vyombo vya dola na wengineo. 


Mfumo wetu mbovu pia naamini ulisaidia mapendekezo ya kubadili utaratibu wa kupatikana mawaziri, kwa kupendekeza wasiwe wabunge ili ipatikane fursa huru ya mawaziri kufanya kazi za Serikali na pia kufika kuhojiwa bungeni wasiwe na masilahi na ubunge.

Binafsi naamini, ili Taifa liweze kubadilika, umefika wakati kutazama upya mfumo wetu wa uongozi ili kutoa fursa watendaji wenye mawazo mapya waweze kufanya kazi.

Hivyo, kama tunataka maendeleo katika Taifa letu ni lazima tukubali kubadili mfumo.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...