Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya (Bongo Fleva), Rashidi Makwiro (29), maarufu kama Chid Benz jana amekiri mahakamani mashitaka matatu yanayomkabili ya kukutwa na Dawa za kulevya aina ya Heroin yenye thamani ya Sh. 38,638, bangi ya Sh. 1,720 na vifaa ya kuvutia dawa hizo kijiko na kigae.
Chid Benz alikiri mashitaka hayo baada ya kusomewa upya hati yake ya mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema.
Hakimu Lema alisema kwa kuwa mshtakiwa amekiri mashitaka yake mahakama yake itasikiliza maelezo ya awali Februari 23, mwaka huu.
Kabla ya kutolewa amri hiyo, Wakili wa Serikali, Diana Lukondo, aliomba kumsomea mshtakiwa mashitaka yake upya. Hakimu aliridhia ombi hilo.
Lukondo alidai kuwa Oktoba 24, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, uliopo Ilala jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa na dawa za kulevya aina ya heroin isivyo halali zenye uzito wa gramu 0.85.
Ilidaiwa kuwa katika shitaka la pili, siku na eneo la tukio la kwanza, mshtakiwa alikutwa na gramu 1.72 za bangi isivyo halali.
Wakili huyo wa serikali alidai kuwa, siku na eneo la tukio la kwanza na la pili, mshtakiwa alikutwa akiwa na vifaa vinavyotumika kuvua dawa za kulevya aina ya heroin, kigae na kijiko huku akijua ni kosa.
Chid Benz alikiri mashitaka yote matatu, atasomewa maelezo ya awali Jumatatu ijayo na dhamana yake inaendelea.
0 comments:
Post a Comment