Kikiosi cha OFM kikifanya uchunguzi kwa wakala magumashi.
Wakati Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikiwasisitiza Watanzania na wamiliki wa kampuni za simu za mkononi kusajili laini zao kihalali ili kila mmoja abaki na taarifa sahihi, kitengo cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publisher mwanzoni mwa mwaka huu kilibaini usajili usiokidhi vigezo unaofanywa na mawakala wa Kampuni moja.
Katika oparesheni hiyo iliyofanyika mitaa kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam, OFM iligundua mawakala hao kutokuwa makini katika kuoanisha taarifa zilizopo kwenye kitambulisho cha mwombaji na kutokujali kwao katika mahitaji ya nyaraka zingine muhimu zinazotakiwa kisheria.
Katika eneo la Mwenge, OFM ilifika kwa wakala mmoja kijana, ambaye baada ya kuombwa kusajili laini ya simu kwa kutumia kitambulisho tu, alikubali na kuanza kazi hiyo bila kujiridhisha kama kitambulisho alichokishika kilishabihiana na aliyehitaji huduma hiyo. Kitambulisho kilichotumika kilitofautiana kwa jina, picha na hata tarehe ya kuzaliwa ya mhusika.
Baada ya OFM kujiridhisha na zoezi hilo, lilimuuliza wakala huyo nyaraka ambazo zinatakiwa kufanikisha usajili huo, lakini wakala alisema kitambulisho peke yake kinatosha kwa zoezi hilo.
Eneo la Buguruni, wakala mmoja wa kampuni hiyo alikubali kusajili laini ya simu ya mteja ambaye hakuwepo kibandani hapo, baada ya kuelezwa na OFM kuwa alikuwa ndugu yao aliyekuwa mbali.
Katika maeneo mengi ambako OFM ilipita, ilibaini kuwa mawakala hao wamekuwa wakiuliza maswali mawili tu ya msingi, hata kwa wateja ambao hawana kitambulisho, juu ya mwaka na tarehe ya kuzaliwa.
Aidha, iligundua baadaye kuwa kampuni wanayoifanyia kazi haina utaratibu wa kuhakiki taarifa zinazowakilishwa kwao na mawakala hao, kitendo kinachowapa kiburi cha kukiuka utaratibu huo, ambao lengo lake kubwa lilikuwa ni kukabiliana na uhalifu unaofanywa kwa kusaidiwa na mitandao ya simu.
Zoezi hilo muhimu, ambalo awali lilimhitaji mwombaji kuwa na kitambulisho cha kazi au barua ya serikali ya mtaa, ikisindikizwa na kitambulisho cha kupigia kura, linafanikishwa kwa mteja kutoa kiasi cha shilingi elfu moja tu.
OFM inatumia fursa hii kuihimiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, kufanya upya uhakiki ili kupata ukweli wa takwimu zilizopo katika mitandao ya simu, kwani upo uwezekano mkubwa wa majina na picha zilizopo huko hazina uhusiano wowote na wenye nazo na hivyo kuwepo kwa uwezekano wa kuhusishwa isivyo halali kwenye matukio ya kihalifu.
0 comments:
Post a Comment