2015-02-03

Lugola kushawishi wananchi wasiichague CCM 2015

              Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola.
 
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola amesema atawashawishi wananchi wasikichague Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba mwaka huu ikiwa serikali haitatekeleza miradi ya kupekeleka maji katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara na hasa jimboni kwake.

Lugola aliyasema hayo jana, wakati akichangia mjadala kuhusu taarifa ya utekelezaji ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na ile ya Kilimo, Mifugo na Maji baada ya kuwasilishwa bungeni jana.

Alisema mradi wa ujenzi wa bomba la maji kutoka Tamau hadi Bunda ambao pia unakusudia kuvipatia maji vijiji vya Bulamba Bizimbwe na Mwisenye umekuwa kizungumkuti kwa muda mrefu sasa.


Alisema inasikitisha kwenye kitabu cha taarifa ya Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Magembe haujaweka mradi huo na badala yake ameweka miradi mingi ya kwenye jimbo lake.

“Na hata kwenye kitabu hiki cha taarifa yake Mheshimiwa Waziri, Hakuna mradi huu wa maji ya Bunda, mradi mkubwa, lakini ukienda kwenye miradi yake ya Same, Mwanga ndiyo imejaa kwenye kitabu hiki, kwa nini nisiamini unafanya kazi kwa kupendelea maeneo yako, ” alisema Lugola.

Alisema wakazi wa Bunda wanahitaji maji hayo kutoka Ziwa Victoria lilipo umbali wa kilometa 20 lakini mpaka sasa ni zaidi ya miaka sita tangu mradi huo uasisiwe hawajapata.

Alisema kwa sasa taifa linaelekea kwenye uchaguzi ambao anaamini CCM kitaendelea kushinda kwa kishindo kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya mawaziri ambayo alitaka sasa yawe ni mabadiliko yenye tija.

Hata hivyo alimtaka Maghembe kufanya mabadiliko haraka ya miradi ya maji kwa kuwa wakazi wa Bunda akiwemo mwenyewe hawatakubali kuipigia CCM kura ikiwa hawatapata maji mpaka kufikia kwenye uchaguzi huo.


“Mheshimiwa Maghembe unao muda wa kufanya mabadiliko wananchi wa Bunda hatutakubali, hatutakubali kupiga kura kwa Chama Cha Mapinduzi, iwe ni udiwani, wabunge, hata mimi nitasema msinipigie kura, haiwezekani zaidi ya miaka sita wananchi wanatumia maji taka, mradi umekwama pesa hakuna,” alisema.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mjumbe wa Kamati hiyo, Said Nkumba alisema halmashauri nyingi nchini zina madeni makubwa kutoka kwa makandarasi hivyo akashauri serikali itoe fedha kwa wakati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Kamati hiyo pia ilipendekeza serikali kuanza utaratibu wa kutumia mita za maji kwenye taasisi zake ili kuepukana na tatizo sugu la kutolipia ankara.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...