2015-02-23

Mbowe atembeza ‘bakuli’ kwa ajili ya kuingia Ikulu anataka kila mwanachama kuchangia Tsh 10,000

Freeman Mbowe
Awataka wanachama wote kuchangia Sh10,000 kwa mwezi.

Mbeya. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza mpango maalumu wa wapenzi na wanachama wa chama hicho kuchangia Sh10,000 kwa mwezi ili kupata fedha za kutosha kukiendesha chama ikwa lengo la kuiondoa CCM madarakani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa njia ya kura.

Mbowe alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia mamia ya wakazi na wafuasi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.

Akifafanua kuhusu michango hiyo kwa kutumia mfano alisema, kama eneo la Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini watapatikana watu milioni moja watakuwa wamechanga kwa mwezi Sh100 milioni ambazo zinatosha kuing’oa CCM katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu. 

Mbowe alisema, Chadema imefanikiwa kuiteka mikoa yote muhimu katika nchi ambayo ipo vizuri kiuchumi na kukubaliwa na wananchi, hivyo njia ni nyeupe kwa upinzani kuingia Ikulu.

Mbowe alisema kutokana na fursa hiyo Chadema kukubaliwa na taifa hili na CCM kupoteza mwelekeo ndiyo sababu ya wao kushinda uchaguzi.

Awali, Naibu Katibu Mkuu Chadema (Zanzibar), Salumu Mwalimu alisema upinzani umejipanga vilivyo na umedhamiria kuingia Ikulu mwaka huu huku akibainisha kwamba mara baada ya kuingia Ikulu jambo la kwanza ni kuwarudishia Watanzania Katiba yao waliyoipendekeza na siyo vinginevyo. 


Wabunge Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ wa Mbeya Mjini na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini, walisema hali ya kisiasa kwa upande wa Chadema katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini umeimairika hivyo kazi iliyopo ni kupata wagombea wenye sifa ya kukubalika na wananchi, muda uliobakia watafanya kazi ya kuzunguka mikoa yote ya ukanda huo.


Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...