MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema), amesema ataendelea kutetea nafasi yake ya ubunge katika jimbo hilo endapo chama chake kitampitisha katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Ndesamburo alitoa kauli hiyo jana katika ufunguzi wa semina ya Baraza la Wanawake wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro (BAWACHA), ambapo alisema chama kisipompitisha yupo tayari kushirikiana na atakayechaguliwa ili jimbo hilo liendelee kubaki mikononi mwa Chadema.
Alisema kumekuwapo na taarifa ambazo zimekuwa zikienezwa na wapinzani wa Chadema kuwa endapo Ndesamburo hatatetea nafasi yake ya ubunge katika jimbo hilo basi litachukuliwa na CCM.
“Hii si kweli na kama sitagombea basi nitahakikisha linaendelea kuongozwa na Chadema, nitakuwa bega kwa bega na atakayechaguliwa kama chama changu kitanitupa pembeni.
“Uchaguzi ni chama, kama kitaniweka pembeni na kumteua mwingine basi nitamsaidia kwa nguvu zangu zote ikiwemo kutumia kiinua mgongo changu chote cha ubunge” alisema.
Ndesamburo ambaye mashabiki wake humwita Ndesapesa alisema Jimbo la Moshi Mjini ambalo linaongozwa na Chadema limekuwa likifanya vizuri hadi kufikia hatua ya kumfurahisha Rais Jakaya Kikwete kwa kumsifu Meya wa Manispaa hiyo, Japhary Michael (Chadema), hivyo lazima liendelee kuongozwa na upinzani miaka mingine ijayo.
Akizungumza katika semina hiyo, Meya wa Manispaa ya Moshi, Japhary Michael alimtoa hofu Ndesamburo kwa kumweleza kuwa hata akiamua kupumzika, jimbo haliwezi kupotea kwani wapo vijana wenye nguvu na uwezo wa kulitetea jimbo hilo liendelee kubaki Chadema kutokana na kazi ambazo zimekwishafanywa.
0 comments:
Post a Comment