KAULI iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, mbele ya Baraza la Maadili lililoketi kumhoji juu ya mgawo wa fedha za Escrow, kuwa alitumia Sh milioni 10 kwa ajili ya kununulia mboga, imeibua hasira kutoka kwa wananchi, wasomi na viongozi wa kada mbalimbali.
Wamesema kauli hiyo ni mwendelezo wa kejeli ambazo zimewahi kutolewa kwa nyakati tofauti na wanasiasa pamoja na baadhi ya viongozi nchini.
Kauli zinazolinganishwa na hii ya sasa ya Tibaijuka kiasi cha kuzua mijadala mikubwa kwenye maeneo mbalimbali, ni zile za hivi karibuni zilizowahi kutolewa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge na aliyekuwa mmiliki mwenza wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira, ambao kwa nyakati tofauti wamepata kuyaita mabilioni yao vijisenti na vijipesa vya ugoro.
Kauli hiyo ya Tibaijuka imeelezwa kuwa ni dharau na dhihaka iliyokosa kipimo kwa Watanzania ambao asilimia 40 wanaishi kwa mlo mmoja kwa siku.
Kwenye mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Instagram, facebook, twitter, blog na mingine, wamehoji kama milioni 10 ni fedha za mboga, kijijini anakotoka Tibaijuka mwenyewe migomba imekufa kwa ugonjwa na mnyauko, huku watu wakiteseka kwa njaa na wengine wakikosa hata Sh 1,000 kwa siku.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, walisema kauli hiyo haipimiki katika mzani wa maisha ya kawaida ya Watanzania.
Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu, Hellen Kijo Bisimba, amesema kauli ya Profesa Tibaijuka ni dharau iliyopita kiwango na inadhihaki asilimia 40 ya Watanzania wote ambao wanaishi chini ya dola moja.
Alisema kauli za namna hiyo ni za kukatisha tamaa wananchi wazalendo ambao wanatumia nguvu yao kubwa kujenga uchumi wa nchi.
“Watu wa namna hii hawajitambui wapo katika kundi gani la jamii wanayoiongoza, hawana uchungu na wavuja jasho na wanadharau kupita kiasi, eti unatumia Sh milioni 10 kwa ajili ya mboga na wakati mwananchi mwingine hana hata Sh 500 ya kumwezesha apate walau mlo mmoja kwa siku,” alisema Dk. Bisimba.
Dk. Bisimba alikwenda mbali kwa kueleza kuwa hata uamuzi ya Baraza la Maadili unaweza kuwa dhaifu kwa sababu haoni sehemu itakayowabana watuhumiwa ili warejeshe fedha walizopewa.
“Ninachokiona au ninachokitarajia juu ya hukumu ya Baraza la Maadili ni sawa na bure, kwa sababu watuhumiwa hawana kazi kwamba watafukuzwa na sidhani kama Baraza la Maadili lina ubavu wa kutengua ubunge wao, ndiyo maana Chenge anawachezea kama watoto wadogo,” alisema Dk. Bisimba.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mwanasheria mmoja ambaye hakupenda jina lake kutajwa gazetini, ambaye alisema japokuwa baraza hilo lina nguvu ya kisheria, lakini halina meno ya kuwakabili watuhumiwa hao.
Pasipo kutoa ufafanuzi wa kina wa kisheria, mwanasheria huyo alisema hukumu ndiyo itakayotanabahisha mitazamo iliyopo kuhusu nguvu ya baraza hilo.
Awali mwanasheria huyo aliizungumzia kauli ya Profesa Tibaijuka kwa kusema kuwa ameyatusi maisha ya Watanzania.
“Angekuwa huko Umoja wa Mataifa kauli yake isingewaudhi wengi kwa sababu alikuwa anaishi na watu wa hadhi yake, lakini kama kiongozi wa wananchi ambao wengi wao ni maskini wa kutupwa, kauli hiyo haistahili na kama Baraza la Maadili litakuwa makini limbane kupitia kauli hiyo,” alisema mwanasheria huyo.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kauli aliyotoa Profesa Tibaijuka ina uasili wa hasira.
Alisema, kwa kuwa mara nyingi wanasiasa wamekuwa wakihukumiwa kabla ya hukumu, mazingira hayo huwajengea hasira, hivyo hujikuta wanatoa kauli mbaya pasipo kutarajia.
“Ukiziweka kwenye mzani kauli ya Chenge, Profesa Tibaijuka na hata ya Rugemalira ambaye ni mfanyabiashara, utabaini kuna kihasira fulani na mazingira ya kauli yao yanatokana na kuhukumiwa kabla ya hukumu, lakini ombi langu ni moja tu, kwamba wanasiasa wanatakiwa wawe wavumilivu, nadhani Lowassa hata Chenge wameonyesha uvumilivu wa kisiasa baada ya kukumbwa na kashifa nzito na zimedumu kwa muda mrefu midomoni mwa watu,” alisema Dk. Bana.
Akitoa mtazamo wake kuhusu Baraza la Maadili, Dk. Bana alisema bado hajaelewa ukomo wa mamlaka ya mwenyekiti wa Baraza la Maadili, hivyo hali hiyo inampa wakati mgumu wa kuzungumzia jambo hilo.
“Napata shida kidogo kujua ukomo wa mamlaka ya mwenyekiti wa Baraza la Maadili, najiuliza kama watuhumiwa watakutwa na hatia ubunge wao utatenguliwa? Je, kama wakitengua vyama vyao au wananchi wataridhia? Hapa ndipo ninapojiuliza kuwa inawezekana nguvu ya Baraza la Maadili si kubwa,” alisema Dk. Bana.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa, alikataa kuzungumzia kauli ya Tibaijuka kwa kusema kuwa haina mashiko katika mustakabali wa Taifa.
“Siwezi kuzungumzia kauli ya mtu wakati kuna ajenda nyingi za kuzungumzia Taifa, binafsi nasubiri hukumu ya Baraza la Maadili,” alisema Dk. Slaa.
Baadhi ya wananchi walipiga simu chumba cha habari kuzungumzia kauli hiyo ya Tibaijuka.
Miongoni mwa wananchi hao ni pamoja na Victor Kabalasa, aliyesema ameshangazwa na kauli hiyo ya Tibaijuka, wakati yeye hiyo milioni 10 hajawahi kuishika hata siku moja tangu azaliwe na sasa ana miaka 43.
Mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la William Kangesha, alisema wakati Tibaijuka akitoa kauli hiyo, kuna watoto wengi wa Kitanzania na Watanzania kwa ujumla wanakufa mahospitalini kwa kukosa matibabu sahihi.
Zaidi alisema wapo mamilioni ya watoto wa Kitanzania ambao mbali na kutokuwa na sare za shule wanatembea peku, wanakaa katika madarasa yasiyo na madawati, dirisha wala milango.
Kauli za kejeli
Mbali na kauli hiyo ya Tibaijuka, kauli nyingine za kejeli zilizopata kutolewa na viongozi na ambazo zimebaki katika vichwa vya Watanzania ni pamoja na ile iliyowahi kutolewa na Rugemalira kwa kusema kuwa alilipwa vijipesa vya ugoro.
“Niliiambia serikali kuwa nyie mmeibiwa na sisi tumeibiwa. Mimi nikawaambia kuwa ‘the end justify the means’ (jambo la muhimu ni matokeo, si njia ulikopitia), mwisho tulikubaliana kwamba kwa masilahi ya Taifa tumalize kesi hii, na mimi ndiyo nikalipwa hivyo vijipesa vya ugoro,” alikaririwa Rugemalira.
Mwaka 2008, aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, alihojiwa na waandishi wa habari juu ya tuhuma nzito za kumiliki kiwango kikubwa cha fedha kinachokadiriwa kuzidi dola za Marekani milioni moja, katika akaunti iliyoko Kisiwa cha Jersey, Uingereza, ambapo alijibu kwa kifupi kwamba fedha hizo kwa viwango vyake zilikuwa ni vijisenti.
Mwingine aliyewahi kutoa kauli ya kejeli ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ambaye alisema kwamba kama kuna watu watashindwa kulipa nauli ya Sh 200 katika kivuko cha Kigamboni, itabidi apige mbizi.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha wa awamu ya tatu, Basil Mramba, naye aliwahi kutoa kauli iliyokera wengi pale aliposema ununuzi wa ndege ya rais ni lazima, hata kama wananchi watakula nyasi.
Miaka ya 1980, John Malecela wakati akiwa Waziri wa Mawasiliano, alitoa kauli ya kejeli akiwa jimboni kwake kwa kusema kwamba, waliokuwa wanahoji ufanisi wa Shirika la Reli (TRC), waende kuzimu.
0 comments:
Post a Comment