2015-02-25

Christopher Alex azikwa katika makaburi ya Nkuhungu,Dodoma


MAMIA ya wakazi wa Dodoma jana walijitokeza kumzika kiungo wa zamani wa timu ya Simba na timu ya taifa, Christopher Alex Massawe (38) aliyezikwa katika 
makaburi ya Nkuhungu mjini hapa huku wachezaji wenzake akiwemo Ulimboka Mwakingwe na Boniface Pawasa wakiangua kilio.Awali katika kuaga mwili wa marehemu, mchezaji aliyecheza naye Simba, Juma Kaseja aligeuka kuwa kivutio kwa mamia ya waombolezaji waliojitokeza nyumbani kwa mama wa Alex, Martha Matonya, eneo la Nkuhungu Bandeko. 
Tukio hilo lilitokea wakati beki aliyecheza naye Simba, Pawasa alipokuwa akiwatambulisha wachezaji waliocheza na Alex na ilipofika zamu ya Kaseja, watu wote walitaka Kaseja aletwe mbele wamwone.

Hata hivyo, baada ya Kaseja kujitokeza alifika mbele akiwa amevalia kofia upande hali ambayo ilizusha minong’ono pamoja na mara kwa mara alionekana kufuta machozi.

Wachezaji waliohudhuria katika maziko hayo ni wale walioitoa Zamalek katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 akiwemo Amani Mbaruku, Pawasa na Kelvin Mhagama.

Alex alifunga penalti ya mwisho iliyokitoa kigogo hicho cha Afrika kwa penalti 5-4.

Wachezaji wengine waliokuwepo mazikoni ni Sadick Bigambo aliyecheza naye CDA, Juma Mazoo ambaye alicheza naye Reli Morogoro, Ulimboka aliyecheza naye Reli Moro na Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ aliyecheza naye Simba na wachezaji wa timu mbalimbali za mkoa wa Dodoma.

Mwakilishi la Klabu ya Simba, Ally Suru ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Mashindano alitoa Sh 500,000 kama ubani.
Miongoni mwa timu alizochezea ni Small Boyz ya Itigi, CDA ya Dodoma, Reli, 
Morogoro, Simba na Taifa Stars. Alex aliyefariki dunia Jumapili asubuhi kutokana na kuugua kifua kikuu, ameacha watoto wawili, Alex na Asnath.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...