Lowassa
Y
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alitoa ufafanuzi huo baada ya waandishi wa habari waliopo katika msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kutaka ufafanuzi wa kinachoendelea mjini Dodoma kwa makundi tofauti kwenda kwa Lowassa kwa madai ya kumshawishi agombee urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Nape akizungumzia suala hilo alisema, “Anachokifanya Lowasa ni kuvunja kanuni na kiburi, ni matendo ya wazi ya kampeni, bila shaka anajua adhabu yake. Matendo hayo yanaweza kumpotezea sifa za kuwa mgombea kupitia CCM.”
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa aliongeza kuwa Lowassa ni miongoni mwa wanaCCM ambao walipewa adhabu na CCM mwaka mmoja uliopita kwa kuanza kampeni kabla ya wakati na mpaka sasa bado wapo kwenye kipindi cha uangalizi wakati vikao husika vikiendelea na tathmini dhidi yao.
Nape alisisitiza kuwa matendo yanayoendelea hivi sasa ni dhahiri kuwa ni kiburi kisicho na maana dhidi ya CCM.
“Lowasa anajua utaratibu wa Chama katika kuwapata wagombea wake kwa ngazi mbalimbali kuanzia udiwani mpaka urais hivyo kuendelea na matendo ambayo yanatafsiri ya wazi kuwa ni kampeni ni kiburi cha wazi. “Kwa matendo hayo ya Lowassa labda dhamira iwe ni kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya Urais kupitia chama kingine na si CCM.”
Nape alisema ni vyema wagombea wa ngazi mbalimbali wakahakikisha wanazingatia Katiba na kanuni za chama hicho ili wasiingie kwenye kundi la kutokuwa na sifa ya kuomba ridhaa ya kugombea udiwani, ubunge na urais.
“Tunaendelea kukumbusha na kusisitiza kwamba wale wote wenye nia ya kugombea kupitia chama chetu kuheshimu kanuni na tararibu za kupata ridhaa kugombea kwa ngazi ya chama chetu,” alisema Nape.
Lowassa amedaiwa kuwa amekuwa akitumia makundi mbalimbali kufanya kampeni ambapo alianza na kikundi cha wajasiriamali jimboni Monduli mkoani Arusha ambapo walienda nyumbani kwake kumuomba agombee.
Hatua hiyo ilifuatiwa na mashehe 50 kutoka wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ambao nao walikwenda nyumbani kwa Lowassa Dodoma kwa lengo la kumshawishi agombee urais.
Baadaye walifuata wachungaji ambao nao walifunga safari hadi nyumbani kwa Lowassa Dodoma na kusema wameamua kumuomba Lowassa agombee urais kwa madai kuwa ana maono makubwa dhidi ya Tanzania.
Baadhi ya wachungaji hao walimwambia Lowassa wanaamini kuwa yeye ndio chaguo sahihi kwao na ndio maana wameamua kufunga safari na kumshawishi huku wakieleza kuwa kila mtu ametumia nauli yake kufika Dodoma.
Kwa upande wake Lowassa, akizungumza na wachungaji hao waliofika nyumbani kwake, alisema anafarijika kuona makundi mbalimbali yakifika nyumbani kwake kumshawishi agombee.
Alinukuliwa na vyombo vya habari juzi akisema pia kuwa hakuna kundi ambalo analituma au kulipa fedha kwa ajili ya harakati za kutaka kugombea urais.
Hata hivyo, tayari baadhi ya makada wa CCM ambao wamo kwenye orodha ya kutaka kugombea urais, wametoa malalamiko yao kuwa kinachofanywa na Lowassa si sahihi.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema kuwa kitendo cha kuandaa watu kwa ajili ya kuanza kampeni si cha kiungwana na kwamba kila mgombea anaweza kufanya hivyo, lakini wanaheshimu kanuni na Katiba za chama chao.
January amenukuliwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii akieleza wazi kuwa anaweza kutengeneza makundi kwa ajili ya kuonesha Watanzania kuwa anahitajika, lakini akasema hizo ni propaganda ambazo hazina tija kwa Taifa.
“Kama mgombea anakubalika kwa Watanzania kwanini atumie fedha nyingi kutafuta makundi ili aonekane anakubalika? Alihoji January katika ujumbe wake aliousambaza katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
0 comments:
Post a Comment