2015-03-10

Ina sikitisha sana:Mume amuua mkewe kwa kumgongelea misumari kichwani kisa ni wivu wa mapenzi

 Happiness Geofrey enzi za uhai wake.
MWANAMUME mmoja aitwaye Boniphace Kiwele mkazi wa Bombambili, Wilaya ya Ilala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam anadaiwa kumuua kwa kipigo na kitu kinachodhaniwa kuwa ni msumari, mkewe Happiness Geofrey (pichani) wiki iliyopita. 

Kiwele alidaiwa kufanya ukatili huo Machi 3, mwaka huu nyumbani kwake baada ya kumtuhumu mkewe kuwa alikuwa kwa mwanaume, tofauti na majirani waliodai kuwa wakati akipigiwa simu mara kwa mara na mumewe na kutakiwa kurejea nyumbani, walikuwa naye katika kikao cha kikundi chao cha vikoba. 

 

Mwili wa marehemu Happiness Geofrey ukiwa ndani ya jeneza.

Mmoja wa majirani ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema Kiwele ambaye ni fundi mchundo (Welding) alimpiga mkewe kwa fimbo ya ufagio ambayo ilikuwa na msumari na kumuumiza sehemu mbalimbali za mwili wake, hasa kichwani.

Jirani huyo alisema marehemu alikuwa pamoja na wenzake wapatao 15 wakijadiliana namna ya kukiendeleza kikundi chao ndipo walipomuona akiinuka mara kwa mara akiongea na simu, akidai ni mumewe anamtaka arudi nyumbani. 




            Ndugu wa marehemu wakiwa wanalia.

“Marehemu alipofika nyumbani alidhani ametoka kwa wanaume na kipigo kilianzia hapo.


“Kwa zaidi ya saa nne alikuwa akipigwa hadi alipopata nafasi ya kuchoropoka na kukimbilia kwa majirani tulimpa msaada wa kumpeleka hospitali, tulimpakiza staili ya mshikaki kwa sababu alikuwa hawezi kukaa, tukaenda FFU Ukonga, ambako madaktari walitutaka tumpeleke Hospitali ya Amana.

“Amana nako madaktari walisema kwa hali aliyokuwa nayo ni vyema tumpeleke Hospitali ya Muhimbili, wakati tunajiandaa kutafuta gari marehemu akakata roho,” alisema jirani huyo, akaongeza kuwa Happiness alifariki Machi 4, mwaka huu saa 3 asubuhi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, SACP Mary Nzuki alikiri kupata taarifa ya tukio hilo. “Ni kwamba mtuhumiwa anasakwa na jeshi la polisi ili afikishwe mahakamani,” alisema.

Marehemu alisafirishwa Machi 7, mwaka huu kupelekwa nyumbani kwao Tabora kwa ajili mazishi.



GPL

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...