Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia (kushoto) akimkabidhi kombe na hundi yenye thamani ya shilingi Milioni 1/- kwa kuwa mchezeji bora wa Mwezi Desemba 2014 wa (VPL) kabla ya mechi kati ya timu yake na Azam FC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa Jumapili. Aliyeshikilia hundi kulia ni Ofisa Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Kaude.
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia (kushoto) akiwa ameshikilia hundi yenye thamani ya shilingi Milioni 1/- ya mchezeji bora wa Mwezi Desemba 2014 wa (VPL), kulia Ofisa Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Kaude.
Na Mwandishi Wetu, Tanga
KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, imemjaza noti kiungo Joseph Mahundi wa Coastal Union baada ya mwishoni mwa wiki kumkabidhi Sh. Milioni 1/-kutokana na kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu.
Mahundi, kiungo fundi aliyekulia kwenye kituo cha Azam FC jijini Dar es Salaam, aliibuka Mchezaji Bora wa Mwezi Desemba 2014 wa VPL akiwa ni mchezaji wa nne kutwaa tuzo hiyo tangu ianzishwe msimu huu na kampuni hiyo.
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia aliyekuwa amefuatana na Ofisa Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Kaude, ndiye aliyekabidhi zawadi hiyo kwa Mahundi dakika chache kabla ya kuanza kwa mechi ya VPL ya Coastal dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa Jumapili.
Baada ya mechi hiyo kumalizika huku Azam FC wakiibuka na ushindi wa bao 1-0, Mahundi aliipongeza Vodacom Tanzania kwa kuanzisha tuzo hiyo.
"Ninawashukuru na kuwapongeza Vodacom kwa kuanzisha tuzo hii kutambua mchango wa wachezaji wanaofanya vizuri VPL. Ninawashukuru pia TFF kwa kuona kutambua uwezo wangu na kunitangaza mshindi wa Desemba. Nitaendelea kujituma zaidi ili nikuze soka langu na kuisaidia Coastal Union," alisema Mahundi.
Matina Nkurlu, Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, alisema kuwa kampuni hiyo itaendelea kutoa zawadi kwa wachezaji wanaofanya vizuri ikiwa ni sehemu ya mikakati na mchango wake katika kuinua kiwango cha michezo, hususan mpira wa miguu nchini.
Tangu tuzo hiyo ianze kutolewa Septemba mwaka jana, ni Coastal Union pekee iliyofanikiwa kutoa wachezaji wawili walioitwaa hadi sasa.
Washindi wa tuzo hiyo tangu ianzishwe ni Antony Matogolo wa Mbeya City (sasa yuko kwa mkopo Panone FC ya Kilimanjaro) aliyeitwaa Septemba, Salum Abubakar 'Sure Boy' wa Azam FC (Oktoba), Rashid Mandawa wa Kagera Sugar (Novemba), Mahundi, Said Bahanunzi wa Polisi Moro (Januari) na Godfrey Wambura wa Coastal Union (Februari).
GPL
0 comments:
Post a Comment