2015-03-31

KUHUSU VURUGU KALI ZILIZOIBUKA MBEYA...........bofya hapa kuona mabomu yakilindima


KUNDI la vijana linalosadikiwa kuwa ni vibaka limeibuka na kufanya vurugu zilizoambatana na uvunjifu wa amani katika eneo la Soweto na Mwanjelwa jijini hapa. 

Kutokana na hali hiyo, Polisi mkoani Mbeya walilazimika kutumia nguvu ya ziada kuwatawanya vijana hao ambao tayari walianza kuweka matairi, mawe na magogo kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam-Zambia katika eneo la Mwanjelwa. 

Kabla ya vurugu hizo baadhi ya wafanyabiashara ambao walikuwa kwenye mgomo wa kutokufungua maduka yao, wakishinikiza kuachiliwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Johson Minja, jana walitaka kufungua maduka yao kisha kuendelea na shughuli zao. 


Wakati, wafanyabiashara hao wakifungua maduka hayo, inasemekana baadhi ya wafanyabiashara ambao wao hawakuwa na utayari wa kufungua maduka, walianza kuwatisha wenzao ambao walitaka kufungua maduka yao. 

Mzozo huo ukiwa unaendelea baina ya wafanyabiashara hao, ndipo kundi la vijana, wanaodaiwa kuwa ni vibaka lilijitokeza na kuanza kufanya fujo zilizoambatana na uvunjifu wa amani. 

Wakizungumza na Mtanzania kwa nyakati tofauti katika eneo la tukio, baadhi ya wafanyabiashara hao, walisema kuwa, wao wameamua kufungua maduka yao baada ya kupata taarifa kutoka kwa wenzao wa mikoa ya jirani kama vile Iringa, Njombe na Ruvuma kwamba wanaendelea na shughuli zao za uuzaji wa bidhaa kama kawaida. 

“Mikoa mingine tayari wafanyabiashara wenzetu wanaendelea na shughuli zao hivyo baada ya kusikia hivyo na sisi leo tumeamua kuja kufungua biashara nzetu, lakini tunashangazwa na hawa wanaofika na kututisha,”alisema mfanyabiashara Edwin Sanga wa Mwanjelwa. 

Akizungumzia vurugu hizo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini alikanusha madai ya kwamba askari walitumia mabomu katika kutuliza ghasia hizo. 

“Tukio hili la uvunjifu wa amani lilitaka kutokea lakini vijana wangu hawajatumia mabomu, silaha wala nguvu ya aina yoyote katika kurudisha hali ya amani, zaidi walichokifanya askari ni kufanya doria katika maeneo hayo ambayo tayari yalionyesha viashiria vya kutokea kwa vurugu,” alisema. 

Alisema, wakati gari hizo za doria zikipita kwenye eneo hilo la tukio na kuweka ulinzi kwenye eneo ambalo tayari vijana waliweka matairi barabarani, wahusika walianza kukimbia wenyewe na mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na vurugu hizo

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...