Dar es Salaam. Watu watano wamefariki dunia kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam, watatu kati yao wakiwamo wanafunzi wawili, wakipoteza maisha baada ya kibanda walichojihifadhi kujikinga na mvua kuangukiwa na nguzo ya umeme na kuwaunguza.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi wa Temeke, Zakaria Sebastian alisema vifo vya watu hao watatu vilitokea katika eneo la Mchikichini Kimbangulile, Mbagala.
Sebastian aliwataja waliokufa kuwa ni Ramadhan Said (10), mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Mchikichini, Alhaji Jumanne (15), mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari ya Charambe na Monica Elistone (26).
Alisema wakati mvua ikiendelea kunyesha, watu hao walijihifadhi kwenye kibanda kilichotengenezwa kwa mabati na ghafla waya wa nguzo hiyo ulikatika na kuangukia kibanda hicho na kushika moto.
“Wakiwa kwenye banda hilo, ghafla nguzo ilianguka na waya wake kuangukia kibanda kilichoshika moto na kuwateketeza watu hao,” alisema Kamanda Sebastian.
Mjumbe wa shina namba nne wa mtaa huo, Kondo Namna alisema zaidi ya nguzo saba zimeinamia kwenye nyumba za watu na wameshatoa taarifa Tanesco, lakini hadi jana, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na shirika hilo.
Wakati huohuo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema wakati mvua zinaendelea kunyesha saa sita usiku wa kuamkia jana, mkazi wa Mwananyamala Edward Warioba (22) alifariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta akiwa amelala nyumbani kwake.
Katika tukio jingine, Kamanda Wambura alisema maiti ya mwanamume mwenye umri wa kati ya miaka 45 na 50 iliokotwa ikielea kwenye makutano ya Mto Goba na Makongo. Alisema huenda mtu huyo alisombwa na maji ya mvua katika eneo ambalo bado halijajulikana. Wakati maafa hayo yakitokea, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuwapo kwa mvua kubwa katika maeneo ya ukanda wa Pwani na kuwataka wakazi wa maeneo hayo kuwa makini.
Mikoa ambayo huenda ikapata mvua kubwa kwa mujibu wa TMA ni pamoja na Lindi, Mtwara, Tanga na Dar es Salaam.
Mamlaka hiyo ilieleza kuwa kutakuwa na mvua inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24 kuanzia jana.
Sababu kubwa ya kuongezeka kwa mvua hizo kunatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua katika maeneo hayo.
0 comments:
Post a Comment