Wachezaji wa Simba wakishangilia goli.
BAADA ya kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Mgambo, vijana wa Msimbazi, Simba, jana waliamka na kutoa kipigo kikali kwa Ruvu Shooting cha mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kutokana na ushindi huo, Simba imefikisha pointi 32 na kuendelea kubaki katika nafasi ya tatu ikiwa ni nyuma ya vinara wa ligi, Yanga ambao wana pointi 37 huku Azam FC wakishika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 36 baada ya nao kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jana.
Simba ilipata mabao yake kupitia kwa Ibrahim Ajibu aliyefunga kwa penalti baada ya Awadhi Juma kuchezewa faulo ndani ya eneo la hatari katika dakika ya 60.Awadhi ambaye aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Abdi Banda, alifunga bao la pili kwa shuti kali lililombabatiza beki wa Ruvu, Hamis Kasanga katika dakika ya 61 na kujaa wavuni.
Elias Maguri ambaye naye aliingia kuchukua nafasi ya Emmanuel Okwi, aliipatia Simba bao la tatu katika dakika ya 75 kwa kumalizia mpira ambao ulitemwa na kipa wa Ruvu, Abdallah Abdallah aliyepangua shuti kali la Said Ndemla.
Licha ya kupata mabao hayo, Simba ilishindwa kutumia nafasi nyingi ilizopata katika kipindi cha kwanza kutokana na washambuliaji wake kukosa umakini.Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema:
“Vijana wangu hawakutumia nafasi vizuri kipindi cha kwanza, niliwapa maelekezo ya nini cha kufanya wakati wa mapumziko na wakayafanyia kazi, tumejipanga kushinda mechi zote zilizosalia.”Upande wa Kocha wa Ruvu, To, Olaba alishindwa kuzungumzia mchezo huo akidai kuwa hakuwa katika hali nzuri.
0 comments:
Post a Comment