2015-03-24

Nature apigia hesabu za mbali ubunge Temeke


                                Juma Kassim Nature

Nature ametoa kauli hiyo huku wasanii wengine wakitangaza nia ya kuwania ubunge majimbo mbalimbali.

Mwanamuziki mwenye uwezo na mvuto jukwaani, Juma Nature amesema kuwa hana mpango wa kugombea ubunge katika Jimbo la Temeke mwaka huu, licha ya awali kutangaza nia hiyo. 

Nature ametoa kauli hiyo huku wasanii wengine wakitangaza nia ya kuwania ubunge majimbo mbalimbali.

Wasanii watakaowania ubunge mwaka huu ni pamoja na Mr II ambaye atatetea ubunge wake wa Mbeya Mjini, Afande Sele, Kalapina, Chopa Mchopanga, JB ambao wametangaza nia zao kupitia vyama tofauti.

Nature ambaye hajawahi kutangaza chama anachokipigia upatu, alisema kuwa ingawa alifuatwa na watu wengi waliomshawishi kugombea nafasi hiyo, lakini atafanya hivyo mwaka 2020.

“Ubunge Temeke, nitapita tu. Wenyewe wanajua kwamba mimi naweza kuwasaidia. Kwa sasa nimewaachia kina Profesa Jay na wengine wachukue nafasi hizo, ila miaka mitano injayo usishangae ukanikuta pale mjengoni nimevaa suti nikiwakilisha wananchi. Kwa sasa sijaamua na malengo yangu ni mwaka 2020,” alisema Nature. 

Alisema kuwa akipata nafasi ya kuwa mbunge, jambo la kwanza kufanya kwa wananchi wake ni kushughulikia kero zilizopo hasa Barabara ya Mbagala.

“Barabara ndiyo kipaumbele, kwani mvua ikinyesha kidogo ni shida, ile hospitali ya Temeke ni ndogo, kumwona daktari ni kazi ngumu. Pia, soko siyo safi, inatakiwa vichimbwe visima na kujengwa vyoo kwani watu wanachafua sana mazingira. Temeke mitaro ni mibovu, mvua ikinyesha ni maafa kwa sababu watu wamejenga kiholela,” alisema msanii huyo.

Alifafanua kuwa wakati wake ukifika atagombea ubunge kupitia chama chochote atakachoona kina msingi mzuri. “Lakini kwa sasa bado sijaona ni chama kipi ngangari,” alisema .



Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...