2015-03-09

PAAA... WAMEKAA



JINA ni Okwi! Okwi! Okwi! Ndilo ambalo lilitawala kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana baada ya Simba kuichapa Yanga kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Awali, hakuna aliyekuwa na uhakika wa kutabiri matokeo, kila mmoja alikuwa na hofu kutokana na timu zote mbili pale zinapokutana kupatikana matokeo ya kushangaza na ndicho kilichotokea jana.

Lakini hili limejidhihirisha tena jana wakati Simba ikiwa haipewi nafasi kubwa kutokana na kiwango chake cha michezo ya nyuma ilipofanikiwa kuibuka na ushindi huo muhimu na baadaye wachezaji wakaonekana kushangilia kwa staili ya kama wanawaambia watani zao: “Mmekaaa..” 

Mengi yalitawala, kadi nyekundu, rafu za hapa na pale, kadi tisa za njano, mashabiki kuzimia na mbwembwe za makocha lakini bado Mganda, Emmanuel Okwi ndiye aliyekuwa shujaa.

Okwi alifunga bao safi la umbali wa zaidi ya mita 20, baada ya kumchungulia kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ na kupiga shuti kali ambalo alilisindikiza kwa macho katika dakika ya 54 ya mchezo.

Okwi ambaye hilo ni bao lake la sita kwenye ligi kuu msimu huu, alikwenda kushangilia upande wa mashabiki wa Yanga ambayo ni timu yake ya zamani kabla hajajiunga na Simba. Bao hilo lilikuwa gumzo kubwa uwanjani hapo kutokana na ubora wake.

Okwi pia inaonekana ni mtaalamu wa kuitungua Yanga kwani tangu mwaka 2011, hilo ni bao lake la tatu kuifunga timu hiyo. Mchezaji mwingine aliyefunga mabao mengi kwenye mechi ya watani tangu 2011 ni Hamis Kiiza aliyekuwa Yanga ambaye pia alifunga matatu.

Yanga sasa inatimiza siku 779 bila kuifunga Simba. Mara ya mwisho kwa Yanga kupata ushindi dhidi ya timu hiyo ilikuwa ni Mei 18, 2013 ambapo ilishinda 2-0.

Hata hivyo, watoto hao wa Jangwani ndiyo walianza kwa kasi ndogo baada ya kuwaacha Simba kutawala kwa dakika kumi na tano za mwanzo.

Hadi dakika ya 13, Okwi alikuwa ameshaotea mara tatu, lakini hadi dakika ya 30 mchezo ulichafuka sana na kuwa na rafu za hapa na pale huku kila mmoja akijifanya mbabe.

Yanga waliona kuwa mshambuliaji wao Danny Mrwanda, anaweza kupewa kadi nyekundu kutokana na jazba na kumtoa nje katika dakika ya 29 tu ya mchezo huo na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu.

Hata hivyo, timu zote zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu, kipindi cha pili ukiacha bao ambalo Yanga wamefungwa lakini hakikuwa kizuri sana kwa Yanga kutokana na kiungo wao mahiri, Haruna Niyonzima, kupewa kadi ya pili ya njano.

Niyonzima alipewa kadi hiyo katika dakika 73, baada ya kupiga mpira wakati mwamuzi akiwa ameshapuliza filimbi kuwa kuna madhambi yamefanyika.

“Nakubaliana na matokeo, lakini sikubali kadi nyekundu aliyopewa Niyonzima, hakika naamini kuwa hakuisikia filimbi ya mwamuzi ndiyo maana akaupiga ule mpira,” alisema Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm baada ya mchezo huo.

Hata hivyo, Niyonzima anaweza kupewa adhabu zaidi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya kuipiga teke meza ya mwamuzi wa akiba wakati akitoka uwanjani.

Katika mchezo huo, timu zote zilifanya mabadiliko kadhaa, ukiacha kumtoa Mrwanda, pia Mrisho Ngassa ambaye hakucheza vizuri alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Kpah Sherman katika dakika ya 77, huku Simba wakimtoa Ibrahim Ajibu na nafasi yake kuchukuliwa na Simon Sserunkuma.

Katika michezo ya msimu uliopita timu hizo zilitoka sare mechi zote baada ya mechi ya kwanza kuwa na matokeo ya 3-3 na ya pili 1-1.

Wachezaji saba ambao ni Ivo Mapunda, Okwi, Ally Mustapha, Mrwanda, Mrisho Ngassa, Amissi Tambwe, Ivo Mapunda na Kelvin Yondani walicheza mchezo wa jana wakiwa wameshazitumikia klabu zote mbili kwa nyakati tofauti. 


“Bao langu nililofunga nalipeleka kwa wanawake wote duniani, kwa kuwa leo ni siku yao muhimu,” alisema Okwi baada ya mchezo huo.

Kwa upande wa K ocha wa Simba, Goran Koponuvic ambaye alionekana kuwa na furaha sana hadi kwenda kushangilia na mashabiki wa Simba alisema kuwa: ”Haya ni matokeo mazuri sana kwetu na hii yote inatokea kutokana na juhudi za wachezaji pamoja na nidhamu ambayo wameionyesha.”

Simba kwa sasa wamefikisha pointi 26 zikiwa ni tano nyuma ya kinara Yanga mwenye pointi 31. 

Simba iliwakilishwa na Ivo Mpunda, Ramadhani Kessy, Mohammed Hussein, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Abdi Banda, Ramadhani Singano, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla na Emmanuel Okwi.

Wakati kwa upande wa Yanga: Barthez, Mbuyu, Oscar Joshua, Nadir Cannavaro, Yodani, Said Juma, Msuva, Haruna Niyonzima, Tambwe, Ngassa na Mrwanda. 
 GPL

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...