2015-03-23

Reina: Asimama golini ligi kubwa nne Ulaya


Ligi hizo ni La Liga (Hispania), Premier League (England), Serie A (Italia) na Bundesliga (Ujerumani).

Kipa wa Bayern Munich ya Ujerumani, Pepe Reina amekuwa wa kwanza katika historia ya soka la Ulaya kucheza katika ligi nne kubwa barani Ulaya.

Ligi hizo ni La Liga (Hispania), Premier League (England), Serie A (Italia) na Bundesliga (Ujerumani). 

Reina (32), ambaye ni raia wa Hispania, wiki iliyopita aliichezea timu yake ya Bayern Munich mechi ya kwanza katika Bundesliga tangu asajiliwe msimu uliopita wakati timu hiyo ilipocheza na Werder Bremen kwenye Uwanja wa Weserstadion.

Katika La Liga, kipa Reina alicheza mechi 100, akiwa na klabu za Barcelona na Villarreal.

Mwaka 2005 alihamia klabu ya Liverpool inayoshiriki Ligi Kuu England na kucheza mechi 284 katika misimu minane. 


Klabu ya Liverpool ilimpeleka Reina katika klabu ya Napoli ya Italia kwa mkopo katika msimu wa 2013/2014 na huko alicheza mechi 29.

Katika msimu uliopita, Reina alichukuliwa na klabu ya Bayern Munich kama mchezaji huru, lakini alikuwa akipata wakati mgumu wa kucheza kwa sababu timu hiyo ina kipa mahiri, Manuel Neuer.

Wiki iliyopita, kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola ambaye ni raia wa Hispania alimpa nafasi ya kucheza Mhispania mwenzake kipa Pepe Reina, hivyo kipa huyo kuweka rekodi ya kucheza ligi nne kubwa barani Ulaya ambazo ni La Liga, Premier League, Serie A na Bundesliga.

Reina ambaye ana watoto watano, ni kipa ambaye akiwa na timu ya taifa ya Hispania alitwaa ubingwa wa Fainali za Kombe la Dunia 2010 na ubingwa wa Ulaya 2008, 2012.

Alipokuwa na Klabu ya Liverpool, alitwaa Kombe la FA msimu wa 2005/06, Kombe la Ligi, 2011/12, Ngao ya Jamii 2006 na UEFA Super Cup, 2005.



Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...