Mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi, jana alitoa ushahidi katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam, kuhusiana na tuhuma zinazomkabili Khalid Kagenzi, za kutaka kumdhuru mumewe.
Kutokana na hatua hiyo ya Mushumbusi, Dk. Slaa alisema tayari wamefunga ushahidi kwa upande wake. Mushumbusi ambaye aliongozana na mumewe, Dk. Slaa walifika katika kituo hicho saa 4:00 asubuhi na kutoka saa 7:25 mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari baadaye, Dk. Slaa alisema alimsindikiza mkewe kituoni hapo kutoa maelezo akiwa shahidi yake.
“Leo mke wangu alikuja kutoa ushahidi. Na maelezo yote aliyoyatoa yameandikwa. Ameyapitia na mimi nimeyapitia. Hivyo, kwa upande wangu ushahidi nimekamilisha. Imebaki kwao tu kwa hatua zaidi pamoja na faili letu kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza: “Ninaomba ieleweke kwamba mke wangu ni shahidi na siyo mtuhumiwa kama ambavyo nimekwisha kueleza. Naomba msipotoshe kama ilivyotokea awali.”
Kwa upande wake, Mushumbuzi alisema wakati tukio linatokea, alishindwa kutoa ushahidi alipoitwa na Jeshi la Polisi kwa sababu alikuwa safarini, lakini baada ya kurudi alitoa taarifa kwa jeshi hilo.
“Wakati tukio linatokea, niliitwa kutoa ushahidi wangu, lakini sikufanya hivyo kwa sababu nilikuwa safari. Niliporudi niliwaambia, kwa hiyo wakaniambia nije leo,” alisema Mushumbusi.
Aliongeza: “Maelezo ambayo nimeyatoa ni yale yale niliyosema kwenye vyombo vya habari. Kwa hiyo yameandikwa na nimeyapitia nikajiridhisha.”
Awali, akizungumza na waandishi wa habari juu ya wito wa mke wa Dk. Slaa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema hakuwa na taarifa na jambo hilo na kwamba suala hilo linawezekana kwa kuwa ni utaratibu wa kawaida wa utendaji kazi kwa jeshi hilo.
“Sina taarifa juu ya jambo hilo. Lakini hilo ni jambo la kawaida. Siyo jambo kubwa sana na ni utaratibu wa kawaida wa utendaji kazi wa polisi. Na kama amekuja kuhojiwa ni wito, ambao anaweza kuitwa mtu mwingine yeyote,” alisema Kova.
Katika maelezo yake kwa vyombo vya habari, Mushumbusi alidai alibaini njama za Kagenzi ambaye alikuwa mlinzi wa Dk. Slaa, kutaka kumuua mumewe baada kukutwa na msaidizi wake wa ndani akiwa katika meza ya chakula, ambayo hutumika kwa ajili ya kuandalia chai ya mumewe japokuwa haikuwa kawaida yake kunywa chai katika meza hiyo.
Alisema hata hivyo, baada ya kukutwa na msaidizi wake wa kazi za ndani, Kagenzi alishtuka na kumwaga chai na hata alipoulizwa sababu za kufanya hivyo, hakutoa sababu za msingi.
Taarifa za awali za Kagenzi kutaka kumdhuru Dk. Slaa zilitolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, mbele ya waandishi wa habari, ambaye alieleza kuwa amekuwa akitumiwa na maofisa 22 wa vyombo vya usalama katika miaka miwili iliyopita kufanya mipango hiyo dhidi ya chama hicho.
Alidai Kagenzi amekuwa akitumiwa na maofisa usalama wa vyombo hivyo kupata taarifa nyingi za Chadema na kuziwasilisha kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Marando alidai mipango hiyo iligunduliwa na kitengo cha usalama cha Chadema kupitia simu za Kagenzi na kwamba, ililenga kuiumiza Chadema kisiasa.
Alidai katika hujuma hizo, Kagenzi amekuwa akiwasiliana na mmoja wa vigogo wa ngazi ya taifa wa CCM.
Marando alidai kuanzia Desemba, mwaka jana, Kagenzi alikuwa amekwishafadhiliwa Sh. milioni saba kwa ajili ya matumizi ya mawasiliano ya simu kufanikisha upatikanaji wa taarifa za Chadema kupitia vikao vyake mbalimbali ikiwamo Kamati Kuu.
Alidai alipohojiwa na Chama, Kagenzi aliwapa kitabu chake cha kutunza kumbukumbu ambacho kinaonyesha mawasiliano kati yake na baadhi ya maofisa wa vyombo vya usalama aliowataja kwa majina na namba za simu zao za mikononi.
0 comments:
Post a Comment