2015-03-23

Simba, Azam mdogo mdogo


Kipa wa timu ya Ruvu Shoooting , Abdullah Abdallah akijaribu kuokoa mpira langoni mwake huku mshambuliaji wa Simba ,Emmanuel Okwi (katikati) akifuatilia wakati wa mchezo wa ligi kuu Tanzaia Bara uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana.Simba ilishinda 3-0.


Timu ya Simba imerudi katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting 3-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Pia, Azam inaipumulia Yanga kileleni baada ya jana kuichapa Coastal Union bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kwa ushindi iliopata, Simba imefikisha pointi 32 na kuendelea kushika nafasi ya tatu huku Azam ikibaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 36 wakati Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 37.

Katika mechi ya jana, Simba ilikubali kulazimishwa na Ruvu kwenda sare mpaka mapumziko lakini katika kipindi cha pili iliamka na kupata bao la kwanza dakika ya 58 ambalo lilifungwa na Ibrahim Ajib kwa mkwaju wa penalti.

Simba ilipata penalti hiyo baada ya Awadhi Juma ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Abdi Banda kuchezewa faulo na Pius Michael katika eneo la hatari.

Dakika mbili baadaye, Awadhi aliipatia Simba bao la pili kwa kichwa huku Elius Maguli akihitimisha mabao ya Simba katika dakika ya 76 baada ya kipa wa Ruvu, Abdullah Abdallah kutema shuti kali la Said Ndemla.

Katika kipindi cha kwanza, timu zote zilicheza kwa kushambuliana kwa zamu, lakini kipindi cha pili Simba ilitulia na kumiliki sehemu kubwa ya mchezo iliyowawezesha kuibuka na ushindi huo.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika, kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema, “Tumepata ushindi wa kishindo, bado tuna uwezo wa kukimbia katika mbio za kuwania ubingwa.”

Katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, bao la Azam lilifungwa na John Bocco katika dakika ya 32 baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Coastal na mpira kumrudia Shomary Kapombe wa Azam aliyepiga shuti na kuwagonga mabeki wa Coastal na mpira kumkuta Bocco aliyeuweka kimiani.

Azam ilitwala mchezo kwa muda mwingi, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kutumia vizuri nafasi walizokuwa wakizipata.

Akizungumza baada ya mechi, kocha msaidizi wa Coastal, Jamhuri Kihwelu alisema, “Nasikitika kufungwa na timu mbovu kama Azam, hawajui kucheza mpira ingawa wana kila kitu, bahati haikuwa yetu.”

Kocha wa Azam, George Nsimbe alisema, “Mimi nautaka ubingwa, haijalishi nimeifunga timu gani, kikubwa ni pointi tatu katika mechi ya Ligi Kuu, hata mechi ijayo nitashinda, ninaamini wachezaji wangu watanipa matokeo mazuri katika mechi zote zilizobaki.”

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...