Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu sita (6) kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya kumiliki silaha kinyume cha sheria, kulima na kukutwa na bhangi pamoja na kuingia nchini bila kibali, kufuatia operesheni inayoendelea Mkoani Dodoma kusaka watuwanaojihusisha na uhalifu wa aina mbalimbali.
Akithibitisha matukio hayo kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME - SACP amewataja watu wanaoshikiliwa na Polisi kuwa ni ERASTO DIHELELA mwenye miaka 31, mkulima, mkazi wa kijiji cha Lukole aliyekamatwa na silaha aina ya Gobore isiyokuwa na namba pamoja na Golori zake 11 na vipande 17 vya nondo akilimiliki bila kuwa na kibali. Mtuhumiwa huyo pia alikutwa amelima bhangi kwa kuchanganya na mahindi katika shamba lake la hekari moja.
Mtu wa pili ni HAPPY GIBSON mwenye miaka 28, mkulima, mkazi wa Kijiji cha Lukole akiwa na silaha aina ya Gobole nyumbani kwake bila kuwa na kibali cha kumiliki silaha hiyo. Vile vile katika kupekuliwa nyumbani kwake mtuhumiwa huyu alikutwa na bhangi kilo tano (5) alizohifadhi ndani ya nyumba yake tayari kwa kusafirisha.
Kamanda MISIME amesema katika oparesheni hiyo pia amekamatwa HAMISI MWIKOLA mwenye miaka 28, mkulima, mkazi wa Kijiji cha Lukole akiwa amelima bhangi kwa kuchanganya ndani ya shamba lake la mahindi hekari mbili.
Watuhumiwa hawa wote wamekamatwa siku ya tarehe 21/03/2015 katika kitongoji cha shuleni mlimani kijiji cha Lukole kata ya Kingiti tarafa ya Kibakwe Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma na watafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu kukamilika.
Aidha Kamanda MISIME amesema wamekamatwa raia wawili kutoka Ethiopia katika eneo la Nala Dodoma Mjini wakiwa hawana kibali cha kuingia nchini na kuishi. Watu hao ni GETHGACHEW ANCHISO mwenye miaka 29, na KONJITI FEYSA mwenye miaka 23.
Vilevile huko katika kijiji cha Tubugwe juu kata ya Chamkoloma Tarafa ya Mlali Wilayani Kongwa amekamatwa mtu mmoja anayefahamika kwa jina la MWAJABU SALUM mwenye miaka 28, mkulima, mkazi wa Tubugwe juu akiwa amelima bhangi ndani ya shamba lake la mahindi la hekari mbili na nusu (2 ½).
Kamanda MISIME ametoa wito kwa wakulima kutolima mazao haramu na badala yake walime mazao yenye tija kwa maendeleo halali kwani hatima ya wahalifu wanaolima bhangi na kukutwa na silaha bila kibali ni kuishia jela na kuzitesa familia zao kwa vitendo wanavyofanya vya kihalifu.
Aidha amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kuwafichua watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, kulima na kumiliki au kuuza dawa za kulevya na kujihusisha vitendo vingine vya kihalifu katika maeneo yote ya Mkoa wa Dodoma kwa usalama wa wananchi kwa ujumla na kutokomeza uhalifu wa aina zote.
Bhangi ikiteketezwa baada ya kukamatwa katika shamba la mahindi.
Watuhumiwa waliokuwa wakilima Bhangi hiyo.
0 comments:
Post a Comment