Baadhi ya Maaskofu wakifuatilia kwa makini tamko lililokuwa linatolewa na wenzao ambao hawapo pichani.
Maaskofu kutoka madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini Tanzania wanakusudia kuonana na mkuu wa jeshi la polisi IGP Ernest Mangu, ili kupata suluhu kuhusu sakata linalomkabili mkuu wa kanisa la ufufuo na uzima, askofu Josephat Gwajima.
Aidha, maaskofu hao pia wameonyesha masikitiko ya kile walichodai kuwa ni vituo vya polisi kutoonekana kuwa ni mahali salama kwa watuhumiwa wa makosa mbali mbali wanaofikishwa hapo.
Askofu Gwajima amelazwa katima hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, alikopelekwa kwa matibabu baada ya kuanguka na kupoteza fahamu wakati akihojiwa na polisi, kwa tuhuma za kumkashifu askofu wa kanisa katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam, Muadhama Kadinali Polycarp Pengo.
Wakizungumza katika mkutano wa pamoja waliouitisha jijini Dar es Salaam leo, maaskofu hso kupitia kwa msemaji wao Damas Mukassa wamesema inasikitisha kuona kuwa mchungaji Gwajima alijisalimisha polisi akiwa mzima na afya njema lakini ghafla akapoteza fahamu na afya yake kuwa mashakani kwa sababu ambazo hazijajulikana.
Katika tamko hilo ambalo linaashiria kutoridhishwa na namna sakata la askofu Gwajima linavyoshughulikiwa, maaskofu hao wameshangazwa na kupinga vikali madai ya polisi kwamba kulikuwa na njama za kumtorosha kiongozi huyo wa kidini ambae katika siku za hivi karibuni habari zake zimekuwa zikipamba vyombo mbali mbali vya habari.
Kwa mijibu wa tamko hilo, njama za kumtorosha askofu Gwajima hazina ukweli wowote ikizingatiwa kiwa alikwenda polisi kwa hiari yake mwenyewe pasipo kushurutishwa na mtu yoyote.
Aidha, imedaiwa pia kuwa hata watu kumi na tano wanaotuhumiwa kuratibu njama za kumtorosha kiongozi huyo ni wafuasi wake wa karibu na ambao aliambatana nao siku ya ijumaa alipojisalimisha kituo cha polisi cha kati, yalipo makao makuu ya polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam.
Kwahiyo katika kuhitimisha tamko lao, maaskofu hao wameazimia kumshauri IGP Mangu aangalie uwezekano wa kuacha swala la Gwajima limalizwe kwa njia na taratibu zinazosimamia imani ya dini ya Kikristo.
0 comments:
Post a Comment