MWANAMKE mmoja mwenye asili ya Kiarabu, Salma Amuri (39) (pichani) mkazi wa Mji Mpya, Kawe jijini Dar, amenusurika kifo baada ya kuchomwa visu sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo tumboni na mumewe aliyetambulika kwa jina moja la Selemani.Mwanaume huyo naye baada ya tukio hilo alijaribu kujiua kwa kunywa sumu, chanzo kikidaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Salma Amuri anayedaiwa kuchomwa visu na mumewe akiwa hoi hospitalini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa chanzo chetu, tukio hilo lilitokea saa saba usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita ambapo mwanamke huyo alijeruhiwa vibaya kiasi cha kufanya utumbo wake kutoka nje, kabla ya ndugu na wasamaria wema kuwachukua wawili hao na kuwakimbiza Hospitali ya Mwananyamala, wote wakiwa mahututi.
Gazeti hili lilizungumza na mwanamke huyo hospitali ambapo alieleza kisa cha tukio hilo.
“Migogoro ndani ya ndoa yetu tuliyofunga miaka ishirini iliyopita na kufanikiwa kupata watoto na wajukuu, ilianza tangu Novemba, mwaka jana baada ya kutembelewa na ndugu yangu aliyekuja Tanzania akitokea Saudi Arabia anakoishi.
“Mume wangu alikuwa ananishutumu kwamba ameambiwa na majirani mimi natembea na huyo mtoto wa mama yangu mdogo, jambo ambalo siyo la kweli kwani hata kiumri, ni mdogo, hajafikisha hata miaka thelathini,” alisema mwanamke huyo.
Moja ya jeraha alolipata mwilini mwake.
“Usiku siku ya tukio saa saba usiku alirudi nyumbani akawa amekaa sebuleni lakini baada ya kumtaka twende tukalale aligoma, mimi nikarudi ndani, mara akaja na kuniambia ameamua kujiua huku akinionesha sumu aliyokuwa ameiandaa kwenye chupa ili anywe.”Aliongeza kuwa alivamiwa ghafla na kushambuliwa kwa kisu kisha alipoteza fahamu akajishitukia akiwa pale hospitali.
Jitihada za kumsikia mumewe ambaye awali naye alikuwa amelazwa kwenye hospitali hiyo, ziligonga mwamba kwa kuwa alikuwa amelazwa chini ya ulinzi wa polisi.Kamanda wa Polisi Kanda ya Kinondoni, jijini Dar, ACP Camillius Wambura alikiri kutokea kwa tukio hilo. “Mumewe alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na hali yake kuwa mbaya na mwanamke yupo Mwananyamala, uchunguzi bado unaendelea,” alisema Wambura.
0 comments:
Post a Comment