Leo katika gazeti hili tuna habari kuhusu vifo vya watu watatu ambao umauti wao unaelezwa kusababishwa na hitilafu ya umeme iliyoanzia kwenye nguzo ya Tanesco.
Ni tukio la kusikitisha kwa sababu miongoni mwa waliokufa ni wanafunzi wawili. Lakini huzuni inaongezeka pale inapobainika kuwa tukio hilo limechangiwa na uzembe wa Tanesco. Kwa mujibu wa Mjumbe wa Shina wa mtaa lilipotokea tukio, Kondo Namna, taarifa za hitilafu hiyo ziliripotiwa kituo cha Tanesco Kurasini tangu Agosti 2, 2014. Lakini tangu wakati huo hakuna matengenezo yaliyofanyika hadi vifo vilipotokea Jumapili.
Kwa mujibu wa Kondo pia zaidi ya nguzo saba zimeinamia kwenye nyumba za watu na wameshatoa taarifa Tanesco, lakini hadi wakati wa tukio hilo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa. Lakini baada ya vifo hivyo shirika hilo lilikwenda kutoa pole kwa wafiwa na baadaye Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema jambo hilo linatakiwa lifanyiwe uchunguzi wa kina na hawezi kuwachukulia hatua wafanyakazi wanaodaiwa kuzembea.
Tunashindwa kumuelewa Mramba anataka uchunguzi wa kina wa nini, wakati ni ukweli kwamba wenye wajibu wao hawakuwajibika ipasavyo. Kuna mfululizo wa matukio mengi yanayotokana na uzembe wa wahusika kutokelekeza wajibu wao ipasavyo.
Aprili 2014 tarafa ya Mang’ula wilayani Kilombero mkoani Morogoro, mtoto Amon Ndawala mwenye umri wa miaka mitano, alikufa baada ya kugusa nyaya za umeme ambapo Tanesco walitaarifiwa lakini walipuuza kurekebisha hitilafu hadi kifo kilipotokea. Kabla ya tukio kuna taarifa kwamba wananchi kwa muda mrefu walilalamikia hatari ya miundombinu ya umeme katika eneo hilo, ikiwamo nyaya za shirika hilo kugusa juu ya paa za baadhi ya nyumba za watu huku nyingine zikigusana na miti ama kuning’inia njiani. Wananchi hao walidai kuwa wamekuwa wakitoa taarifa za mara kwa mara kwa viongozi wa shirika hilo kuhusiana na mazingira ya hatari ya miundombinu ya Tanesco, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kurekebisha.
Agosti 2013 huko Mbalizi mkoani Mbeya, nyaya za umeme zilizokuwa zimening’inia mita moja kutoka usawa wa ardhi, zilisababisha kifo cha Neema Kipenya (26), baada ya kuteleza na kushika nyaya hizo kwa lengo la kujinusuru asianguke. Tukio hilo lilielezwa kusababishwa na uzembe wa kutoziondoa nyaya hizo na kuziacha hapo kwa miezi kadhaa.
Julai 2013 wilayani Hai mkoani Kilimanjaro eneo la Sadala, kijana aliyefahamika kwa jina la Valerian Mosha alikufa baada ya kunaswa na umeme uliotokana na kulegea kwa nguzo ya Tanesco na kusababisha nyaya zinazopitisha umeme kuwa kimo cha chini. Hayo ni matukio machache kati ya mengi ambayo yamesababisha vifo kutokana na uzembe wa wafanyakazi wa Tanesco, ama kwa makusudi au kwa sababu wanazozifahamu wenyewe.
Leo mkurugenzi wa Tanesco anaibuka na kusema hawezi kumchukulia hatua mfanyakazi wake, hadi uchunguzi wa kina ufanyike. Ni uchunguzi gani anaoutaka Mramba, zaidi ya taarifa zilizotolewa kuhusu dharura na kushindwa kufanyiwa kazi na watendaji wake?
Tunahoji kitengo cha dharura cha Tanesco kina kazi gani? Tabia ya wafanyakazi wa Tanesco ya kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati inatoka wapi? Ni nani wa kuwajibika kutokana na uhai wa Watanzania kupotea bila sababu? Kwa nini viongozi wa Tanesco wanashindwa kuwachukulia hatua wafanyakazi wazembe?
0 comments:
Post a Comment