VITA ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kati ya Yanga na Azam inatarajiwa kuendelea tena leo, pale timu hizo zitakapoteremka kwenye viwanja tofauti kusaka pointi tatu.
Yanga, ambao ni vinara wakiwa na pointi 40, watakuwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini hapa, wakivaana na Wagosi wa Kaya, Coastal Union, mchezo unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake.
Mabingwa watetezi wa ligi, Azam FC, wenye pointi 36, wataikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex, mchezo unaotarajiwa kukumbushia historia ya msimu uliopita pale timu hizo zilipotoa sare ya mabao 3-3 na kuonyesha burudani safi ndani ya dimba hilo.
Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kutinga raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwa kuichapa mabao 5-2 FC Platinum ya Zimbabwe, vile vile Yanga imeshinda mechi tatu zilizopita za ligi.
Kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Yanga iliweza kuifunga Coastal kwa bao 1-0, bao lililofungwa na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa kichwa.
Coastal Union, inayoshika nafasi ya tano kwa pointi 24, haijafanikiwa kushinda mchezo wowote tokea Februari 28, mwaka huu, ilipoifunga Mgambo JKT bao 1-0, hadi inakutana na Yanga leo imeambulia sare mbili dhidi ya Kagera Sugar (2-2) na Ruvu Shooting (1-1) pamoja na vipigo viwili ilipocheza na Azam (1-0) na Tanzania Prisons (1-0).
0 comments:
Post a Comment