JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemtaka Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kupeleka nyaraka 10 za mali anazomiliki.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwanasheria wa Askofu Gwajima, John Mallya, alisema anatakiwa kuzipeleka nyaraka hizo kituoni hapo Aprili 16 mwaka huu.
Mallya alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya mteja wake kuhojiwa na polisi kuhusu tuhuma zinazomkabili za kumtolea maneno ya kashfa hadharani Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Alisema mahojiano yaliyoanza saa saa 1:14 asubuhi hadi saa 6:45 mchana jana yalitawaliwa na maswali ya kumtaka aeleze mali zake anazozimiliki ikiwamo helkopta pamoja na historia ya familia yake.
“Polisi walitaka kujua ukoo wa baba na mama yake, ndugu zake waliofariki dunia na kujieleza lugha ya matusi anayodaiwa kutoa hadharani dhidi ya Kardinali Pengo,” alisema Mallya.
Alisema baada ya mahojiano hayo polisi walimtaka Askofu Gwajima kupeleka nyaraka 10 zikiwamo hati ya helkopta, hati ya usajili wa kanisa, orodha ya wajumbe wa Bodi ya Baraza wa Wadhamini wa Kanisa, idadi ya makanisa anayomiliki na matawi yake.
Alitaja nyaraka nyingine anayotakiwa kuiwasilisha kuwa ni muundo wa utawala wa kanisa,waraka wa maaskofu, return za kanisa, hati za kanisa, nyumba na mali za kanisa pamoj na mpigapicha za video za kanisa.
“Nyaraka zote hizo ametakiwa kuziwasilisha Aprili 16 katika kituo cha Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam saa 2:00 asubuhi,”alisema mwanasheria huyo.
Awali Askofu Gwajima alisema polisi walimwita leo (jana) kuendelea na mahojiano baada ya kuyasimamisha kutokana na kutetereka kwa afya yake hivi karibuni.
“Mahojiano yameendelea vizuri na yamemalizika salama, lakini mengine mtaambiwa na wanasheria wangu,” alisema Askofu Gwajima.
Askofu huyo alifika kituoni hapo akiwa ameongozana na msaidizi wake Gwandu Mwangasa na mwanasheria wake, Mallya huku akitembea kwa kuchechemea.
Ilipofika saa 1:30 Naibu Kamishna Msaidizi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro, aliwaita waumini zaidi ya 20 wa askofu huyo walikuwapo kituoni hapo na kuwauliza maswali mbalimbali.
Siro: Mmekuja kufanya nini?
Waumini: Tumekuja kwa ajili ya askofu wetu.
Siro:Ninachofahamu ni kwamba Askofu Gwajima ameshapewa hati yake ya kusafiria kwenda kutibiwa nje ya nchi, hivyo hapa amekuja tu kuripoti ataondoka.
Gwajima yupo katika mikono salama nendeni mkafanye kazi za uzalishaji… nyie mtakaa hivyo hivyo bila kuzalisha?…mtazalisha saa ngapi kila siku mpo polisi?
Waumini: Sisi tupo akiondoka tunaondoka naye.
Siro: Makubwa haya…!
Baada ya kutamka maneno hayo aliondoka huku akicheka.
Muda ulivyokuwa unazidi kwenda wafuasi hao walikuwa wakiongezeka katika kituo hicho hadi wakafikia zaidi ya 200 huku baadhi yao wakionekana kuvalia vizibao vilivyoandikwa mgongoni ‘Polisi Jamii’.
Hao walilisogelea lango la kuingilia kituoni hapo na kusimama hapo kama walinzi.
Katika mahojiano ya awali, Machi 27 mwaka huu, Askofu Gwajima alizimia na kukimbizwa katika Hospitali ya Polisi katika Muhimbili kabla ya kulazwa TMJ Dar es Salaam.
Siku tano baadaye askofu huyo aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo huku akiwa anasukumwa katika kiti cha kubeba wagonjwa(wheel chair)kabla ya kuombewa siku ya Pasaka na wachungaji kutoka Japan.
Baadaye aliweza kusimama na kutembea.
0 comments:
Post a Comment