2015-04-10

Zitto Kabwe Asema Kitendo Cha kuitwa MSALITI Ni Mbinu Zinazotumika Kumuua Mwanasiasa wa Upinzani

Kiongozi wa chama cha ACT-Tanzania,Zitto Kabwe amesema kuitwa msaliti ni mbinu zinazotumika 'kumuua' mwanasiasa wa upinzani nchini.

Amesema mwanasiasa wa upinzani akitakiwa kuuawa kisiasa si jambo geni kusikia anatuhumiwa kutumika na Usalama wa Taifa au Pandikizi la Chama cha Mapinduzi, CCM.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dae es Salaam juzi,Zitto alisema kauli kama hiyo ilitumika kumshusha kisiasa mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA, Mabere Marando na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.

"Si jambo jipya, mmesahau kwamba Mbatia aliitwa pandikizi,leo Mbatia yuko wapi,si yuko meza moja na UKAWA?

"Mmesahau baada ya serikali ya Umoja wa kitaifa juzi tu hapa kwamba CUF waliitwa CCM-B, mmesahau kwamba CUF waliitwa mashoga, leo kiko wapi?

"Mmesahau Marando aliitwa pandikizi, tena dhidi ya Mrema(Mwenyekiti wa TLP),leo Marando ni shujaa na Mrema tunamtukana.Hizi ni siasa tu na zitaendelea tu," alisema

Aidha alisema kuna watu wengine wataibuka baadaye nao wataanza kulaumiwa, kama Mwalimu Nyerere alivyosema.....Ukishakula Nyama ya Mtu Huachi.

Kutokana na hali hiyo alisema, walioitwa wasaliti wametoka huko walikokuwa na watasikika wasaliti wengine wanaibuka kwa sababu siasa iko hivyo..

"Juzi nimemsikia Halima Mdee anasema mimi siyo ACT,ninyi mliwahi kuandika kama Halima ni ACT,hiyo maana yake nini,inamaanisha kuna presha anapigwa huko.

"Angalau Shibuda ni mtu ambaye haeleweki misimamo yake ni nini, lakini hivi ni vitu vya kawaida,"alisema.


Akizungumzia kutumiwa na vyombo vya usalama,Zitto alisema yeye kama kiongozi hawezi kuacha kuwasiliana na watu wa usalama wa Taifa.

"Huwezi kuwa kiongozi wa chama kikubwa kinachojiandaa kushika dola usiwe na uhusiano na Mkuu wa Jeshi la Polisi,Mkuu wa jeshi la wananchi au Mkuu wa Usalama wa Taifa,utakuwa ni kiongozi wa ajabu sana." Alisema

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...