2015-04-10

Askari wa JKT Auawa Wakati Akisaidiana na Polisi Kuyakabili Majambazi Yaliyokuwa Yamepora Fedha Iringa


Watu wawili akiwemo jambazi mmoja na askari mwanafunzi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wamekufa na wengine kunusurika kuuawa katika tukio lililotokea juzi, mjini Mafinga mkoani Iringa wakati majambazi wakirushiana risasi na askari wa Jeshi la Polisi.

Risasi hizo zilipigwa wakati Polisi hao wakijaribu kuokoa fedha za mfanyabiashara Salama Semwaiko zilizoporwa na majambazi wawili waliotumia pikipiki wakati wakifanya uporaji huo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema mfanyabiashara huyo aliporwa fedha hizo juzi majira ya saa 2.45 asubuhi alipokuwa akitoka nyumbani kwake kwenda kwenye biashara zake.

Tukio hilo la kusikitisha lililovuta hisia za watu wengi na kufanya baadhi kuzimia wengine kukimbia hovyo na kujifungia ndani kwa ajili ya kuokoa maisha yao lilitokea katika eneo la Kinyanambo B, nje kidogo ya mji wa Mafinga.

Kamanda Mungi alisema; “mfanyabiashara huyo akiwa katika gari lake akielekea kwenye biashara zake mjini Mafinga, mfanyabiashara huyo alisimamishwa na mtu mmoja aliyekuwa amevaa koti jeusi na baada ya kusimama alimtolea silaha na kumtaka atoe fedha na vitu vyote vya thamani alivyokuwa navyo .” 

“Baada ya kuona hana msaada mfanyabiashara huyo alijikuta akilazimika kutoa Sh 700,000 alizokuwa nazo, simu ya mkononi na baadaye ilitokea pikipiki ambayo haikufahamika namba za usajili na kumpakia mtu huyo na kuanza kukimbilia eneo la Kinyanambo,” alisema.

Alisema mara baada ya majambazi hao kutoweka, Jeshi la Polisi lilipewa taarifa na kuwahi eneo la tukio na kwa kushirikiana na wananchi walianza kuwakimbiza majambazi hao na ndipo majibizano ya risasi yalipoanza. 

Katika hekaheka hiyo, Kamanda Mungi alisema Said Ngudi (25) ambaye ni askari wa JKT Makutupora, Dodoma alipigwa risasi na kufa papo hapo wakati akisaidia kupambana na majambazi hao.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...